Nini Kitaendelea kwa ‘Screen Protector’ Baada ya AFCON?

Nini Kitaendelea kwa ‘Screen Protector’ Baada ya AFCON?


Nini kitaendelea kwa Djigui Diarra baada ya AFCON? Najiuliza hapa. Napenda namna ambavyo Baraka Mpenja anavyomtangaza uwanjani. Jinsi alivyomtungia jina la Screen Protector. Anafanana na jina lake. Anajua kweli namna ya kulilinda lango lake. Kwa kila kitu. Kuanzia mikono hadi miguu.


Huku miguuni Diarra ni kipa wa ‘Pep Guardiola’. Anajua kutumia miguu yake kwa ufasaha katika mfumo mpya wa soka la kisasa walilotuletea hawa makocha wapya kwamba eti lazima kipa ajue kutumia miguu yake kwa ufasaha. Juu ni mzuri katika michomo. Ni kipa aliyekamilika hasa.


Juzi alikuwa langoni kwa mara ya tano mfululizo wakati timu ya taifa ya Mali ilipotolewa na Ivory Coast katika hatua ya robo fainali michuano ya Afcon 2023. Ilibakia dakika moja tu Diarra aonyeshe uwezo wake katika mikwaju ya penalti, lakini kwa bahati mbaya wenzake wakazubaa akafungwa.


Kuna hofu imeanza kutanda kwa mashabiki wa klabu yake hapa nchini. Huenda Diarra akawa ameonwa na klabu mbalimbali kubwa ndani na nje ya bara la Afrika, hivyo akajikuta amechomoka nchini bila ya Yanga kupenda. Hofu hiyo pia wanayo mashabiki wa Simba kwa beki wao wa kati, Enock Inonga.


Hakuna kilichonishangaza kuhusu uwezo wa Diarra. Hata hivyo, nina wazo la namna gani Diarra alishuka huku Afrika Mashariki badala ya kwenda juu Ulaya. Klabu aliyokuwa anachezea pale Mali ni kubwa. Stade Mallen. Ni miongoni mwa klabu kubwa nchini humo. Lakini kuna mawakala wengi wanaozunguka Afrika Magharibi kusaka vipaji.


Sidhani kama Diarra hakuonwa. Alionwa. Kilichotatiza nadhani ni kimo chake. Wenzetu walioendelea katika mchezo huu wanajali sana kuhusu kimo cha kipa pamoja na mabeki wa kati. Wanaweza kufanya masikhara na nafasi nyingine za uwanjani, lakini sio nafasi hizo mbili. Wanahitaji watu warefu katika nafasi hizo.


Inabidi uwe na uwezo uliopitiliza kuweza kucheza nafasi hizo huku ukiwa na futi za Diarra. Labda ndio maana Diarra alikuja huku kwetu na hakutiliwa maanani sana na mawakala pamoja na klabu mbalimbali za Ulaya. Vinginevyo ni kipa wa kisasa ambaye ana utaifa unaombeba ambao ungeweza kumpeleka mbali kwa urahisi tu.


Zaidi ya kila kitu, katika michuano hii Diarra ameendelea kuonyesha ubora wake wa kutumia miguu kama makocha wa kisasa wanavyotaka. Kama wakija kuangalia mikanda yake ya video katika mechi anazocheza ligi yetu na mechi mbalimbali za kimataifa akiwa na Yanga, watagundua kitu hiki hiki. Ni zaidi ya David de Gea linapokuja suala la kutumia miguu yake vyema.


Michuano hii imempaisha. Hatua aliyofikia imempaisha. Wakati wenzake watakuwa wakipanda ndege kurudi katika klabu zao mbalimbali za Ulaya, yeye atakuwa akisafiri kurudi Afrika Mashariki kuichezea Yanga. Sidhani kama ni bahati mbaya sana. Kuna kitu kinasimama nyuma ya yeye kuwepo nchini.


Kitu kilicho wazi ni tayari Diarra alikuwa bora akiwa nchini kwao. Sio kwamba amekuwa bora akiwa hapa. Tayari alishakuwa mchezaji wa timu ya taifa tangu wakati akiwa Mali. Michuano hii imempaisha tu lakini tayari Diarra alishakuwa bora muda mrefu na ilishangaza kuja huku kama tatizo sio la kimo kama ninavyofikiria.


Sasa ni suala la kuona kama michuano hii inaweza kumpatia timu kwingineko. Kama tatizo sio kimo chake basi huenda michuano hii ikawa imefungua milango ya Diarra kucheza nje ya bara hili. Ukiona bado yupo hapa hapa basi fahamu kimo ni kikwazo kwa Diarra.


Mawakala wanaokuja katika michuano hii huwa wanakuja kwa sababu mbili. Sababu ya kwanza ni kuangalia vipaji vinavyocheza ndani ya Afrika. Hawa ni wachezaji wachache zaidi kwa sasa kwa sababu wachezaji wengi wanaoshiriki michuano hii wanacheza soka la kulipwa Ulaya na wana mikataba madhubuti.


Tayari wachezaji hawa wanafahamika kwa klabu mbalimbali za Ulaya. Wanaotazamwa zaidi ni hawa kina Diarra na Inonga. Hawa wanaingia katika kapu moja pamoja na mastaa kama wa Mamelodi Sundowns ambao wanaipaisha Afrika Kusini kwa sasa. Lakini kuna mastaa wa Taifa Stars ambao wengi wanacheza ndani. Hawa ndio kina Ibrahim Bacca.


Wateja wanaweza kuwa wawili. Kuna klabu mbalimbali za Ulaya na Asia, lakini kuna wateja wa ndani ya Bara la Afrika. Hawa ndio wale ambao wamekuwa wababe katika soko letu kwa miaka nenda rudi. Timu za Afrika Kaskazini. Kina Al Ahly, Raja, Wydad, Zamalek, RS Berkane, Far Rabat na wengineo.


Kama Yanga hawataki kumuuza Diarra basi bahati yao kubwa itatokana na ukweli klabu za Afrika Kaskazini zimekuwa hazina utaratibu wa kununua makipa. Kwa mfano, Misri ni marufuku kuleta kipa kutoka nje. Ni sera yao. Wao wanahitaji zaidi washambuliaji na viungo wa chini wa shoka kama kina Himid Mao.


Lakini kama wazungu na watu wa Asia wakimhitaji Diarra basi Yanga watakuwa na wakati mgumu zaidi. Wasifu wake umeshajitoleza. Kuipeleka Yanga fainali za Shirikisho na kuipeleka Mali hatua ya robo fainali huku akiwa kipa namba moja na mwenye uwezo mkubwa wa kutumia miguu yake ni wasifu tosha kumchukua katika klabu zao.


Kwa sasa ni wakati wa kusubiri na kuona nini kitaendelea kwake. Ni wakati wa kujua ukweli kama kweli ni kimo ndicho kilichomgandisha Mali na kisha Tanzania kwa muda mrefu. Akiondoka tunaweza kuamini kimo hakikuwa kikwazo. Akibaki basi tutaendelea kuamini kimo kimekuwa kikwazo kikubwa kwake.


Rafiki yetu wa zamani, Marcio Maximo alipokuja nchini na kumfanya Juma Kaseja kuwa kipa wa pili nyuma ya Ivo Mapunda yalizuka maneno mengi kutoka kwa mashabiki ambao daima waliamini Kaseja alikuwa juu ya Ivo kwa uwezo. Hata hivyo, Maximo alikuwa anatuma ujumbe tu wa wazungu kuhusu suala la kimo.


Kabla ya hapo miaka mingi nyuma aliwahi kuja kocha wa kizungu wa Taifa Stars aliyempeleka beki mahiri wa kati wa wakati huo, George Masatu kwenda kucheza kama beki wa kulia akimpisha beki wa Sigara, Abuu Juma aliyekwenda kuwa beki wa kati. Aliona kimo kilikuwa kikwazo kwa Masatu kucheza katikati. Watu hawakumwelewa.


Ni kweli zipo kesi za makipa wafupi. Zipo kesi za mabeki wa kati wafupi. Hata hivyo, huwa ni chache katika soka la nchi zilizoendelea kisoka. Wazungu hawaamini kama kipa mwenye kimo cha Diarra anaweza kuruka hewani kwa usahihi na Erling Haaland wa Manchester City hata kama akinyoosha mikono yake. Tusubiri kuona hatima ya Diarra.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad