Mashabiki wa Yanga wanatamba kama kuna mtu imara katika ukuta wa kumlinda kipa Djigui Diarra, anayesubiri kucheza robo fainali ya Afcon, basi ni beki Ibrahim Bacca, lakini Simba wanasonya na kutaja kitasa cha gharama kinachowapa heshima kimataifa, Henock Inonga anayesubiri rekodi kama ya kipa huyo, Ivory Coast.
Inonga naye yupo robo fainali ya Afcon 2023 kama ilivyo kwa Diarra akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo, lakini sasa namba za beki huyo wa Simba na Bacca aliyekuwa na timu ya taifa, Taifa Stars zinashtua.
Mabeki hao wa kati ambao aina ya uchezaji wao inafanana kwa kiasi kikubwa, wamekuwa gumzo katika fainali hizo za Afcon kutokana na kiwango bora walichoonyesha kiasi cha kuanza kupapatikiwa sokoni na timu tajiri za barani Ulaya na Afrika Kaskazini zikiwatolea macho kinona kutaka kuwasajili.
Hapa chini ni rekodi za wachezaji hao kuanzia katika Ligi Kuu Bara hadi kimataifa na kuonyesha walistahili kabisa kugombewa, na sio ajabu ikitokea wakiibukia katika klabu nyingi kama zenye fedha zitaamua kufanya mambo.
LIGI BACCA FRESHI, INONGA ATIBULIWA
Bacca amefanikiwa kuichezea Yanga mechi tisa za ligi kati ya 11 ambazo timu hiyo imecheza huku mechi mbili ambazo amezikosa ni kutokana na mzunguko wa makocha kwa nafasi yake kuchukuliwa na Dickson Job.
Inonga akiwa kwenye ligi amefanikiwa kuanza kwenye mechi sita akikosa nne za timu yake iliyocheza mechi 10, ambapo kati ya hizo nne alizokosa tatu alilazimika kuzikosa kufuatia kuumia vibaya kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union aliotolewa uwanjani.
BACCA MABAO 6, INONGA 10
Utulivu wa ukuta wa Yanga na hata makali ya Bacca yambeba pia beki huyo ambapo kwenye mechi ambazo ameichezea Yanga kwenye ligi ameruhusu mabao sita huku Inonga akiruhusu 10.
Kwenye Ligi ya Mabingwa, Inonga alimuacha Bacca ukuta wake wa Simba ukiruhusu mabao matano katika mechi nane ambazo alicheza Mkongomani huyo ukiondoa zile mbili za African Super League huku Bacca akiruhusu sita kwenye mechi sita ambazo alicheza kati ya nane ambazo Yanga ilicheza.
BACCA KASHINDA 13, INONGA 8
Upande wa ushindi Bacca ambaye msimu huu ameongeza mkataba wa miaka miwili kusalia katika timu hiyo amefanikiwa kushinda mechi 13 ambapo kati ya hizo tisa ni zile za ligi huku nne za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Inonga akiwa na Simba amefanikiwa kuiongoza kushinda mechi tano za ligi kati ya sita alizoanza huku upande wa Ligi ya Mabingwa akipata ushindi mmoja pekee Wekundu hao walipoifunga Wydad Athletic nyumbani.
AFCON INONGA JUU, BACCA CHALI
Inonga anasubiri kucheza robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika atakapokutana na Guinea, beki huyo akikosa kuanza mchezo mmoja pekee ambao nao aliingia kipindi cha pili, huku Bacca akiishia hatua ya makundi na kikosi cha Taifa Stars akianza mechi zote, lakini wakiwa hawachekani kwani hakuna ambaye amefanikiwa kuvuna ushindi ndani ya dakika 90 ya mechi zote walizocheza.
UCHEZAJI SAWA
Makali ya mabeki hao katika ukabaji ni kama wanaringana kwani sio rahisi kukatiza mbele yao kwa mipira ya juu au ile ya ‘takolingi’ ambazo zimekuwa zikiwabeba
WASIKIE WADAU
Akiwazungumzia mabeki hao, nyota wa zamani wa Simba, Fikiri Magoso alisema unapozungumzia mabeki bora wa kati kwa sasa Ligi Kuu Bara hutaacha kuwataja Bacca na Inonga anaoamini watafika mbali.
“Unapoona wachezaji wanaitwa timu za taifa ni ishara wana kitu kikubwa wamekionyesha katika klabu zao. Sasa kwangu naona wote hawana tofauti kwani kama ni kuanzisha mashambulizi wanaweza, kukaba na kuwania mipira ya juu,” alisema Magoso aliyewahi kuwika pia na Reli Morogoro.
Kipa wa zamani wa Simba, Yanga, Azam na Taifa Stars, Ivo Mapunda alisema hashangazwi na viwango vinavyoonyeshwa na wachezaji hao.
“Mchezaji mzuri siku zote hupimwa katika michuano ya kimataifa sasa ukiwaangalia wote wameonyesha ni kwa jinsi gani ni muhimu kuanzia klabu wanazocheza hadi timu ya taifa kwa sababu wanapata nafasi na wanazitendea haki uwanjani,” alisema Ivo aliyewahi kuwika na Prisons, Moro United na Go Mahia ya Kenya.
Beki wa kati wa zamani wa kimataifa aliyewahi kutamba na Pamba, Simba na Taifa Stars, George Masatu alisema jambo kubwa wanalolifanya nyota hao ni kutumia fursa za kutangaza zaidi vipaji vyao, kwani wanapoonyesha viwango ni sehemu ya kuonekana huku akiwataka kutobweteka bali wazidi kupambana.