Aliyekuwa Beki wa Wekundu wa Msimbazi ‘Simba SC’ Pascal Wawa, amewaonya mabeki wa timu hiyo kwa kuwataka kuwa makini na safu ya ushambuliaji ya Asec Mimosas.
Jumamosi (Februari 24) Simba SC itashuka dimbani nchini Ivory Coast kucheza mechi yao ya Mzunguuko wa tano dhidi ya Asec Mimosas ikiwania nafasi ya kufuzu hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Wawa raia wa Ivory Coast aliyezichezea Simba SC, Singida Fountain Gate FC na sasa yupo nchini kwao, amewang’ata sikio Wekundu wa Msimbazi akiwataka mabeki wa timu hiyo kuwa makini na safu ya ushambuliaji ya wapinzani kwani ni hatari, kutokana na kucheza pasi fupi fupi za kuwachanganya na kuwachosha wapinzani, wanapokuwa na mpira kuelekea kufanya mashambulizi.
Amesema mara chache hubadilika kulingana na kasi ya mpinzani, hivyo Simba SC wanatakiwa kuwa makini hasa safu ya ulinzi kuhakikisha hawatoi nafasi ya kushambuliwa hasa kipindi cha kwanza kuruhusu bao.
“Nawafahamu Simba SC vizuri hasa inapokuwa kwenye mechi za kimataifa, wako vizuri, ninaamini wakiwa makini safu ya ulinzi na washambuliaji wakitumia nafasi zinazopatikana, nina matumaini makubwa watapata ushindi hapa Ivory Coast,” amesema Wawa.
Simba SC ilianza hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa sare ya 1-1 dhidi ya Asec, ikasuluhu mbele ya Jwaneng Galaxy, ilifungwa 1-0 dhidi ya Wydad AC na kushinda 2-0 ilipopambana na Wydad.
Katika msimamno wa Kundi B, Simba SC ipo nafasi ya pili kwa pointi tano nyuma ya Asec yenye Pointi 10 kileleni, Jwaneng Galaxy ina pointi nne wakati Wydad ikiburuza mkia na alama tatu ambapo timu zote zimeshacheza mechi nne kila moja.