Wananchi wakiwamo wastaafu na waliotekeleza miradi katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, wamejitokeza hadharani wakilalamika kutolipwa.
Malalamiko hayo wameyatoa jana Jumatatu Februari 5, 2024 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika stendi ya mabasi ya Nkasi, mkoani Rukwa uliohutubiwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda.
Makonda aliyetokea mkoani Katavi yupo wilayani humo kuimarisha uhai wa chama hicho na kusikiliza kero za wananchi. Alimuondoa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, William Mwakalimbile kwenye mkutano akawalipe wadai wa halmashuri hiyo.
Akipokea kero za wananchi, alijitokeza Catherine Siame na kusema anadai halmashauri hiyo, Sh 4milioni za malimbikizo ya mshahara.
Siame amesema alistaafu utumishi wa umma mwaka 2020, lakini Mei mosi, 2019 alipandisha cheo, licha ya hatua hiyo hakuwahi kupewa stahiki zake hadi sasa.
"Namdai mkurugenzi fedha zangu za malimbikizo ya mishahara ya miezi 17," amesema Siame.
Makonda akamuuliza Siame alipoenda kwa mkurugenzi aliambiwa nini naye akajibu, alimwambia hana majibu.
Kwa kauli hiyo, Makonda alimuita Mwakalimbile, ambaye amesema madai ya watumishi ni mengi na yameshapelekwa ofisi ya utumishi kwa hatua zaidi.
"Haya ni masuala ya mishahara yanalipwa na utumishi," amesema Mwakalimbile.
Makonda amehoji iwapo amewahi kumjibu Siame, naye akasema: ‘Tumeshawaambia wastaafu wote.’
Hata hivyo, mkurugenzi huyo amesema hajawahi kumuona au kuzungumza na Siame isipokuwa maelekezo yake yalikuwa kwa wastaafu wote.
Siame amedai mkurugenzi amekaidi maelekezo ya Serikali yaliyotolewa mwaka 2023 yakimtaka alimpe fedha zake.
Mwakalimbile amesema waraka wa Serikali kuhusu malipo ya Siame yakionyesha ana haki ya kulipwa stahiki zake baada ya kustaafu.
Mwakalimbile alimuomba Makonda alichukue suala hilo kwa ajili ya utekelezaji.
"Ofisini hamkai, watu hamsikilizi au kwa vile hawana ndugu? Tangu mwaka 2020 suala hili halijafanyiwa kazi, lakini ulivyokuwa unajibu ulikuwa unajiamini kweli,” amesema Makonda na kuongeza:
“Unafungua ofisi leo unamlipa mama (Siame) apande kwenye gari lako sasa hivi. Mama tafuta gari la Mwakalimbile upande sasa hivi, dereva wa mkurugenzi mpokee mama hapo."
Makonda ameuliza mwingine mwenye kero, ndipo alipojitokeza Simon Ndago. Amesema amefanya kazi katika kituo cha afya cha Nkomolo lakini alilazimika kuuza nyumba ili kulipa deni alililokuwa akidaiwa na mafundi wenzake.
Ndago amesema anaidai halmashauri Sh8 milioni baada ya kutekeleza ujenzi huo miaka sita iliyopita.
Mwakalimbile amesema madai yote ya wazabuni wameshayachukua, jambo ambalo halikumfurahisha Makonda akisema anatoa majibu ya jumla.
Hata hivyo, Mwakalimbile alimuomba Makonda kwa mara nyingine alichukue suala hilo kwa ajili ya utekelezaji.
"Mzee gari la mkurugenzi linakuhusu," amesema Makonda.
Ilikuwa vivyo hivyo kwa mwananchi mwingine aliyesema anaidai halmashauri Sh100 milioni baada ya kujenga nyumba ya mkurugenzi, ofisi ya mipango na madarasa ya shule ya sekondari ya Nkasi.
Makonda alimuuliza Mwakalimbile gari lake linabeba watu wangapi? Akajibu wanne akiwemo yeye.
“Sasa wewe tafuta gari la kupanda, mama akae mbele, wengine nyuma mkamalizane, katika mkutano wangu sitaki kashughulike na madeni ya watu," amesema Makonda.