Phiri wa Simba Aingia Penyewe, Power Dynamos Wampa Makaratasi

Phiri wa Simba Aingia Penyewe, Power Dynamos Wampa Makaratasi


Mashabiki wa Simba bado wamekunja roho kutokana na kitendo cha mabosi wa klabu hiyo kuwatoa kwa mpigo washambuliaji wawili, Jean Baleke na Moses Phiri katika dirisha dogo la usajili lililofungwa katikati ya mwezi uliopita, licha ya kushushwa mashine mpya za kuziba nafasi zao.


Sasa unaambiwa baada ya Baleke kupata timu huko Libya, Mzambia Phiri yeye ameibukia kwao akijiunga na Power Dynamos na siku chache baada ya kumwaga wino, nyota huyo aliyeondoka Msimbazi akiwa ameifungia timu hiyo jumla ya mabao 16 yakiwamo 13 ya Ligi Kuu Bara na mengine matatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika amevunja ukimya kwa kuzungumza na Mwanaspoti kutoka Zambia na kuchimba mkwara.


Nyota huyo wa zamani wa Zanaco, aliyewahi kuwaniwa na Yanga kabla ya kuibukia Simba msimu uliopita amesema amerudi kwenye utawala wa Ligi Kuu Zambia na kilichobaki kwake ni kuonyesha alichonacho.


Phiri amejiunga na timu hiyo kwa mkopo wa miezi sita akitokea Simba kuchukua nafasi ya Thomas Chideu aliyeenda Green Eagles na licha ya kukataa kuzungumzia chochote kuhusu Tanzania, kwa madai ameshafunga faili hilo, amekiri kumalizana na timu hiyo.


Nyota huyo amesisitiza bado ana uwezo wa kufanya vizuri na anaiona nafasi yake ndani ya timu hiyo atafanya kile kilichompeleka ikiwa ni pamoja na kujiweka kwenye ushindani.


"Ligi ya Zambia ni mwenyeji nayo nafahamu ushindani wao, siingii kama mgeni kazi yangu ni kufanya kazi kwa kuhakikisha naonyesha utofauti na waliopo kwa kufanya kwa ukubwa," amesema Phiri aliyefunga mabao matatu tu msimu huu katika Ligi Kuu kabla ya kulazimisha kuondoka Msimbazi kutokana na kukosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kocha Abdelhak Benchikha.


"Hilo linawezekana kwani bado naamini nipo kwenye nafasi hiyo ya kufanya vizuri licha ya changamoto za hapa na pale lakini nina imani kubwa ya kufanya kitu ambacho mkitarudisha jina langu kwenye washambuliaji wanaofanya vizuri," ameongeza nyota huyo aliyefahamika zaidi kwa jina la Jenerali kutokana na staili yake ya kushangilia kwa kupita saluti kama afande.


Akizungumzia maisha mapya akiwa na Power Dynamos, Phiri amesema ana kazi kubwa ya kufanya kuwathibitishia waajiri hao wapya kwamba hawajakosea kumpa nafasi, huku akitamba anaamini katika kujituma, hivyo hana wasiwasi kwani uzuri anacheza uwanja wa nyumbani na wenyewe wanamjua.


Phiri ameondoka Simba msimu huu akiwa tayari amecheza dakika 278 kwenye mechi tisa ikiwa ni wastani wa dakika 31 kwa mchezo akifunga mabao matatu tu na ilielezwa mapema alikuwa akiomba kuondoka katika dirisha hilo ili kupata timu itakayompa nafasi kucheza kwa muda mrefu.


Kabla ya kuangukiwa na majanga, Phiri alianza na mguu mzuri Simba msimu uliopita akifunga mabao 10 katika Ligi Kuu Bara na mengine matatu katika mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Big Bullets ya Malawi, alifunga mawili ugenini na moja nyumbani kabla ya kuumia Desemba 3 mwaka juzi na kuwa nje kwa muda mrefu na kupoteza namba katika kikosi cha kwanza chini ya kocha Roberto Oliveira 'Robertinho', aliyeichukua timu kutoka mikononi mwa Juma Mgunda aliyekuwa akimtumia mara kwa mara.


Hali yake ilizidi kuwa mbaya hata alipokuwa Abdelhak Benchikha kutoka Algeria na kupata nafasi ya kusajiliwa kwa mkopo huko Zambia huenda ikawa nafasi yake ya kurudisha ufalme aliokuwa nao zamani Zanaco kabla ya kuamua kujiunga na Simba iliyoizidi ujanja Yanga iliyokuwa ikimnyemelea pia.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad