Jeshi la Polisi, limetoa ufafanuzi wa taarifa iliyo ripotiwa katika baadhi ya vyombo vya Habari ambayo ilikuwa na kichwa cha habari kisemacho, kashfa Polisi yahusishwa na kutekwa kwa Baba na mwanawe.
Akitoa taarifa hiyo leo Januari 31, 2024 Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, Kamshna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, David Misime amesema taarifa hiyo iliwataja waliopotea kuwa ni Damas Bulimbe na mwanaye Lucas waliopotea toka Novemba 15, 2023.
Amesema, Baba huyo alimdhamini mtoto wake kutoka katika Kituo cha Polisi Kakubilo kilichopo Busanda Mkoa wa Geita, alikokuwa akishikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya shangazi yake aitwaye Nyamiti Bulimbe Novemba 8, 2023.
SACP Misime ameeleza kuwa, kwa mujibu wa uchunguzi uiofanywa na Jeshi hilo hadi sasa familia hiyo, ipo kwenye uhasama mkubwa kutokana na mgogoro wa kugombea shamba lililoachwa na Bulimbe Mswaga aliyefariki dunia.
Ameongeza kuwa Polisi inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kwa kushirikisha na maafisa toka makao Makuu, ili kubaini na kupata ushahidi wa watu waliohusika katika Mauaji ya Nyamiti Bulimbe.
Aidha, amesema Jeshi la Polisi litaendelea kuchunguza kwa karibu taarifa zote za watu waliopotea ambazo zimetolewa, ili ukweli upatikane.