Rais wa Zanzibar , Dr Mwinyi |
Rais Mwinyi "Waziri Kama Una Baa, Alafu Pombe Imezuiwa na Serikali Sema"
Rais wa Zanzibar, Dr. Hussein Mwinyi amewataka Mawaziri wanaojiuzulu wawe wakweli badala ya kutoka na kwenda kuwaaminisha Watu kinyume chake na kutolea mfano kwamba kama Waziri anamiliki Baa alafu pombe zimezuiliwa na Serikali basi aseme wazi kwamba hatua hiyo imeingilia maslahi yake.
Akiongea leo February 01, 2024 wakati akiwaapisha Mawaziri wapya Ikulu Zanzibar, Rais Mwinyi amesema “Uwaziri sio nafasi ambayo utakaa nayo maisha kuna njia nyingi ambazo zitakutoa kwenye Uwaziri, aidha utaondolewa au utawajibika kwa tatizo litakalotokea, unapochukua sekta hizi ujue kuna matatizo yanayoweza kutokea na matatizo hayo wala si lazima usababishe wewe na pale ambapo haukubaliani na Serikali sema na kuwa muwazi tutakuheshimu zaidi, kama una baa Watu wamezuia pombe sema Mimi nina baa inaingilia na maslahi yangu, kuwa muwazi"
“Sababu nyingine ya Waziri kujiuzulu ni pale ambapo Serikali inaamua jambo na wewe hukubaliani nalo, unatoka unajiuzulu kwasababu hukubaliani na maamuzi yaliyotolewa na Serikali lakini kuna jambo moja lazima tukumbushane wakati unawajibika kwa njia yeyote ile ya kwanza au ya pili ni lazima uwe mkweli na ukweli ninaozungumzia hapa ni kama kuna mgongano wa maslahi, kama tumezuia kitu na wewe una biashara hiyo tangaza, sema ukweli, sema ukweli hapa kuna mgongano wa kimaslahi Mimi ni muagizaji wa kitu fulani na nyinyi mmezuia lakini ukitoka halafu ukaenda kuwaamisha Watu kinyume chake si sahihi"
Kauli ya Rais Mwinyi inakuja siku chache baada ya aliyekuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Mohammed Said kurekodi video fupi akitangaza kujiuzulu nafasi yake ya Uwaziri akisema mazingira ya kutekeleza jukumu hilo yamekuwa magumu ikiwa pia ni siku kadhaa tangu alipoviambia vyombo vya habari kuwa kuna athari zimeanza kujitokeza na kuzua sintofahamu ya kurudisha nyuma biashara ya Utalii Zanzibar baada ya uwepo wa uhaba wa pombe katika Hoteli na Migahawa.