Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, imeahirisha mchezo kati ya Simba na Mtibwa uliokuwa umepangwa kupigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Huu ulikuwa mchezo wa 16 kwa timu hizo wa Ligi Kuu Bara baada ya mzunguko wa kwanza kumalizika jana, Simba ikimaliza nafasi ya pili na pointi 36 na Mtibwa ikiwa mkiani na alama nane.
Taarifa ya bodi imesema sababu ya kuahirishwa kwa mchezo huo ni kuipa Simba nafasi ya kufanya maandalizi ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ya makundi dhidi ya Asec Mimosas, utakaopigwa Ijumaa Februari 23, kwenye Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny nchini Ivory Coast.
Simba inayoshika nafasi ya pili kwenye Kundi B, ikiwa na pointi tano inatakiwa kushinda mchezo huu ili ifufue matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Kwa mujibu wa chanzo kutoka Simba, timu hiyo itaondoka Jumanne, Februari 20 kwa ajili ya mchezo huo muhimu kwao.