Baadhi ya Watanzania mitandaoni wanasema kwamba sanamu mpya ya kumuenzi mwasisi wao Julius Nyerere haifanani naye.
Sanamu hiyo ilizinduliwa Jumapili nje ya makao makuu ya Umoja wa Afrika katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa.
"Najua ishara ni muhimu zaidi lakini sura ya sanamu haifanani kabisa na Mwalimu Nyerere akiwa mzee au kijana," Maria Sarungi anasema kwenye X (zamani Twitter).
Nyerere alikuwa kiongozi wa Tanzania tangu uhuru wa taifa hilo mwaka 1961 hadi 1985.
Alikuwa mwafrika aliyepigania mshikamano wa Afrika na miongoni mwa wapigania uhuru waliopinga utawala wa wazungu wachache kusini mwa Afrika.
Mwaka jana, sanamu ya heshima ya Rais wa kwanza wa Zambia, Kenneth Kaunda, ilibidi kuondolewa baada ya wiki kadhaa za kejeli, huku watu vivyo hivyo wakisema kwamba haikufanana naye.