Yanga imemaliza kazi kwenye Ligi Kuu Bara na sasa akili za kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi zimehamia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, akipata mzuka mwingi baada ya Al Ahly ya Misri na CR Belouizdad kutoka suluhu na kutangaza vita mapema kwa Waalgeria akisema watakufa nao Kwa Mkapa.
Jana usiku CR Belouizdad ikiwa nyumbani mjini Algiers, Algeria ililazimishwa suluhu hiyo mbele ya watetezi na vinara wa Kundi D, Al Ahly na kuishusha Yanga hadi nafasi ya tatu ikisaliwa na pointi tano kama walizo nazo Waalgeria hao, huku Wamisri wakisalia kileleni na pointi sita baada ya kila moja kucheza mechi nne.
Sare hiyo imempa mzuka mwingi Gamondi na kutamka kuwa kwa sasa hali ilivyo kwenye kundi ni lazima kila mtu ashindwe mechi zake ili kuamua timu mbili za kwenda robo fainali na kwamba baada ya kumalizana na KMC jana mjini Morogoro, moja kwa moja ameanza mipango ya mechi ijayo dhidi ya Waalgeria hao waliowafumua 3-0 ugenini.
Kocha Gamondi alikiri suluhu ya jana usiku imelifanya kundi kuwa gumu zaidi, lakini imekuwa nafuu kwao tofauti kama na Waalgeria hao wangeshinda kwao au kupoteza mbele ya Al Ahly.
“Kundi letu limekuwa gumu zaidi na kwa sasa kila atakayechanga vizuri karata zake ndiye atakayepata nafasi ya kutinga hatua inayofuata kwa mechi mbili zilizobaki. Bahati nzuri tunaanzia nyumbani na mchezo huo ujao tunaupa kipaumbele, kwani ni kama fainali kwetu,” alisema Gaomni alipozungumza na Mwanaspoti baada ya mechi ya Algeria.
“Hakuna urahisi wowote kwetu kwa matokeo yaliyotokea jana (juzi) tunachotakiwa kukifanya sasa ni kuhakikisha tunapambana kwenye mechi ijayo ili kupata matokeo mazuri na bahati nzuri vijana wanajua mtihani tulionao.”
Kocha huyo kutoka Argentina, alisema kwa sasa kwa mechi zilizosalia hakuna hesabu za vidole, ila kilichobaki ni kupatikana kwa matokeo kwa kila mchezo ulio mbele huku akisisitiza kuandaa mbinu sahihi ili kuiwezesha timu kufikia malengo wakianza nyumbani Februari 24 kwa kuikaribisha CR Belouzdad.
Alisema hana kazi rahisi kuweza kufikia mafanikio hayo, huku akiweka wazi kuwa ana kibarua kigumu kuweza kufikia malengo hasa akiumizwa na matokeo mazuri ya aliyemtangulia, Nasreddine Nabi.
“Kila kocha ana malengo mazuri kwenye timu anayopewa majukumu naamini ubora wa kikosi nilichonacho tunaweza kufanya mambo makubwa na ya kushangaza kama ilivyo kuwa hatua ya makundi,” alisema.
“Hakuna aliyekuwa anaamini tunaweza kufika huko sasa tunacheza hatua hiyo. Tulianza vibaya kwa kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao lakini baadaye tukarudi mchezoni na kupambana, tutaendelea pale tulipoishia.”
Alisema sio rahisi kufuzu hatua inayofuata, lakini mbinu na kupambana kwa wachezaji alionao anaamini kila mmoja atafanya kitu kutokana na ubora.
Yanga ikimalizana na CR Belouizdad itasafiri hadi Misri kuumana na Al Ahly ambao walitoka nao sare kwenye mechi ya kwanza iliyopigwa mwaka jana jijini Dar es Salaam, vijana hao wa Gamondi wakilazimika kuchomoa bao jioni kupitia Pacome Zouzoua baada ya Percy Tau kuitanguliza timu hiyo.
Kama Yanga itaibuka na ushindi itaifanya ifikishe pointi nane, huku CR Belouizdad ikisaliwa na tano, ilhali ikiombea matokeo ya ushindi kwa Al Ahly dhidi ya Medeama ya Ghana inayoburuza mkia, ili iwe na kazi nyepesi ugenini kwani Wamisri watakuwa wamejihakikisha kufuzu robo fainali na kuwaachia msala na Waalgeria kuwania nafasi moja iliyosalia.