Dar es Salaam. Baada ya mijadala ya muda mrefu kuhusu uhalisia wa sanamu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere iliyozinduliwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU), Serikali imeibuka na kueleza kuwa sanamu hiyo imezingatia vigezo vya kitaalamu na inaakisi kwa asilimia 90 taswira ya kiongozi huyo.
Hatua hiyo imetokana na mitazamo ya watu mbalimbali hasa kwenye mitandao ya kijamii, wakikosoa utengenezaji wa sahamu hiyo wakieleza kwamba, halina taswira halisi ya Mwalimu Nyerere.
Katika ukosoaji huo, pia zimehusishwa sanamu zingine mbalimbali zilizowahi kutengenezwa na kusimikwa sehemu tofauti nchini, huku nyingi zikionekana kutoakisi taswira halisi ya Mwalimu Nyerere.
Hata hivyo, wataalamu wa sanaa hiyo waliohojiwa na Mwananchi hivi karibuni wameonyesha dosari katika uchongaji wa sanamu hizo, wakisema pengine hazikufuata kanuni za uchongaji na ufinyanzi.
Sababu zatajwa kinachosababisha Sanamu la Mwalimu Nyerere kukosewa
Ufafanuzi wa Serikali kuhusu sanamu hiyo umetolewa Ikulu jijini Dar es Salaam leo Alhamisi, Februari 22, 2024 na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa.
Balozi Mussa ametoa ufafanuzi huo wakati akijibu swali la mhariri wa habari msaidizi wa Mwananchi, Ibrahim Yamola aliyehoji Serikali inazungumziaje maoni ya wananchi kuhusu sanamu hilo.
Katika majibu yake hayo, Balozi Mussa amesema utengenezwaji wa sanamu hilo umehusisha kamati maalum iliyoundwa, ikihusisha wadau mbalimbali, ikiwemo familia ya Baba wa Taifa.
Serikali yaingilia kati sakata la Sanamu ya Mwalimu Nyerere AU
“Kamati ilikuwa na watu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), familia ya Mwalimu Julius Nyerere (Madaraka Nyerere), Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,” amesema.
Baada ya kutengenezwa kwa sanamu hiyo, kamati hiyo imeridhika kwamba linafanana na Mwalimu Nyerere na hata mtoto wa kiongozi huyo (Madaraka), alikiri ina taswira ya baba yake.
“Kauli ya mwanawe Madaraka Nyerere ameitoa mara kadhaa na hadi siku ya uzinduzi nilikuwepo pale mjini Addis Ababa (Ethiopia), akasisitiza kuwa yule ni baba yake na kama kuna mtu anabisha amuulize yeye,” amesema.
Katika utengenezaji wa sanamu hilo, amesema Serikali imefuata maelekezo ya kitaalamu yaliyotolewa na kamati hiyo iliyoshiriki tangu mwanzo hadi mwisho chini ya ufadhili wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Hata hivyo, amesema vigezo vya utengenezaji wa sanamu za viongozi vinataka liwe na taswira ya angalau asilimia 70, lakini sanamu la Mwalimu Nyerere lina asilimia 90 ya vigezo.
Akifafanua zaidi, Balozi Mussa amesema sanamu hilo linaonyesha taswira ya Baba wa Taifa katika miaka ya 1960 hadi 1980 na si kama wengine wanavyofananisha na picha yake ya miaka ya 1990.
Amewataka wanaokosoa sanamu hilo, wajikite katika vigezo vilivyotumika vya kitaalamu, badala ya kuishia kuzungumza bila ushahidi.
“Naomba sana mtoe maelezo ya kisayansi na mnaweza kumuona Madaraka au kamati,” amesema.
Rais Samia Suluhu Hassan alizindua sanamu ya Mwalimu Nyerere Februari 18, 2024 kwenye ofisi za AU akiwa ameambatana na Rais mstaafu Jakaya Kikwete na Madaraka Nyerere.
Tukio hilo lilishuhudiwa na viongozi wengine wa mataifa mbalimbali ya Afrika, lengo likiwa ni kutambua mchango wa Mwalimu Nyerere kwenye harakati za ukombozi barani Afrika.