KIKOSI cha Simba kinajiandaa kuondoka nchini kwenda Ivory Coast kuwahi pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya ASEC Mimosas utakaopigwa Ijumaa hii, huku timu hiyo ikirahisishiwa kazi baada ya wenyeji kutokuwa na huduma ya mshambuliaji anayoongoza kwa mabao kwenye mechi za makundi, Sankara Karamoko.
Nyota huyo aliyekuwa akihusishwa na Yanga katika dirisha dogo la Januari na kukwama dakika za mwisho kisha kuibukia klabu ya Wolfsberger AC ya Austria, ameondoka ASEC akiwa na rekodi tishio jambo linaloweza kuleta faida kwa Simba katika mchezo huo, japo kocha Abdelhak Benchikha amevunja ukimya na kusema hababaishwi kwa hilo.
Simba inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kujihakikishia nafasi ya kutinga robo fainali, kwani hadi sasa imekusanya pointi tano ikiwa nafasi ya pili nyuma ya ASEC Mimosas inayoongoza na 10 ikitangulia hatua ya robo fainali kutoka Kundi B.
Iko hivi. Hadi anaondoka Sankara ndiye aliyekuwa kinara wa mabao wa Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa amefunga manne na kuchangia moja (asisti) kati ya saba iliyofunga timu hiyo, akiwa ametumia jumla ya dakika 89 tu kwa michezo minne iliyocheza Asec katika hatua hiyo ya makundi.
Kukosekana kwa nyota huyo ni faida sana kwa Simba ambayo inaingia katika mchezo huo, huku ikiwa na kumbukumbu ya sare ya 1-1, mechi ya kwanza zilipokutana Kwa Mkapa Novemba 25, mwaka jana, ambapo Sankara aliingia kipindi cha pili dakika ya 76 akichukua nafasi ya Moise Kabore na dakika moja baadaye aliasisti bao la Serge Pokou.
Mchezo na Jwaneng Galaxy ulioisha kwa ASEC kushinda mabao 2-0, Desemba 9 mwaka jana, alicheza dakika 45 na kufunga yote mawili huku kwenye marudiano yaliyopigwa Desemba 19, alicheza kwa dakika moja na kufunga bao katika ushindi wa 3-0.
Mechi na Wydad Casablanca ambayo ASEC ilishinda bao 1-0, Desemba 2, mwaka jana Sankara aliingia dakika ya 64 akichukua tena nafasi ya Kabore na kufunga dakika ya 72, hivyo kuonyesha alivyokuwa muhimu na kukosekana kwake kunaweza kuipa faida Simba.
Hata hivyo, licha ya faida hiyo ambayo Simba inaenda kuipata huenda isiwe rahisi kwani rekodi zinaonyesha katika mechi mbili za michuano ya CAF ilizokutana na Asec ugenini haijawahi kushinda na mara ya mwisho kwenye makundi ya Kombe la Shirikisho misimu miwili iliyopita, ilifungwa mabao 3-0 mechi iliyopigwa Machi 20, 2022.
Msimu huo, Simba ilimaliza nafasi ya pili katika kundi ‘D’ na pointi 10 sawa na RS Berkane ya Morocco iliyokuwa kinara ila zikitofautiana mabao ya kufunga na ASEC ikimaliza ya tatu na pointi tisa wakati US Gendarmerie ikiburuza mkia na pointi tano.
Hata hivyo, kocha Benchikha alisema kama benchi la ufundi na wachezaji kiujumla wanatambua umuhimu wa mechi hiyo kwani matokeo mazuri ndiyo yatakayowaweka sehemu nzuri ya kusonga hatua inayofuata.
“Tunacheza na timu nzuri ndio maana wapo sehemu walipo sasa, hatupambani na mchezaji mmoja kwa sababu tunachokiamini wapinzani wetu wanacheza kitimu zaidi hivyo tunajipanga kuhakikisha kila nafasi tunayopata tunaitumia vizuri,” alisema kocha huyo raia wa Algeria.