Sugu Amshukia DC Kuhujumu Maandamano Chadema

 

Sugu Amshukia DC Kuhujumu Maandamano Chadema

Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ametumia takriban dakika tano za hotuba yake, akidokeza kile alichokiita figisu za kuzuia mkutano wa hadhara wa chama hicho, huku akimtaja Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Benno Malisa kuwa mmoja wa waliohusika.


Hata hivyo, alipotafutwa Malisa kuzungumzia kauli hiyo alisema ameisikia na anasubiri taarifa rasmi, huku akifafanua kuwa maandamano hayo yaliruhusiwa na Rais Samia Suluhu Hassan na ndiyo maana hakuna aliyezuiwa kushiriki.


 Alisema hata Naibu Waziri Mkuu, Dk Dotto Biteko kugongana nao kwenye msafara, alitumia busara katika kuwapisha njiani kutekeleza ‘4RS’ ya Rais Samia, akiahidi baada ya kupata taarifa rasmi ataielezea zaidi.


“Nimesikia ila sijapata taarifa rasmi, lakini maandamano yalifanyika na hakuna aliyezuiwa kwa sababu tayari walishapewa kibali na Rais Samia, hivyo hayo mengine tusubiri,” alisema Malisa.


Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Ruanda Nzovwe, baada ya wanachama na wafuasi wa chama hicho kufanya maandamano yaliyohusisha safari ya kilomita 30.4 kutokea maeneo mbalimbali mkoani Mbeya, Sugu alisema,“namuonya DC Benno Malisa, amewaita bajaji wote leo kule Mkapa ili wasiwepo hapa, sasa Malisa kwa bahati mbaya sana anapenda bata, anapenda kuzurura kwenye maeneo yetu.


“Tutampiga marufuku asitembee usiku kama ataendelea kutuingilia kwenye masuala yetu ya siasa Mbeya Mjini.”


Hata hivyo, Sugu akizungumzia msafara huo wa Dk Biteko alisema alipaswa kuambatana nao ili awaeleze wananchi wa Mbeya lini watapata umeme.


“Sisi hatuna tatizo naye, alitakiwa aje hapa, tumkaribishe kama Naibu Waziri Mkuu, ili kupitia umma huu wa Mbeya awaambie Watanzania ni lini watapata umeme wa uhakika,” alisema Sugu. Maandamano Chadema


Jana, siku ya kazi haikuwa kikwazo kwa wafuasi wa Chadema Mkoa wa Mbeya, kujitokeza kwa wingi kushiriki maandamano yaliyoandaliwa na chama hicho.


Maandamano hayo ni mwendelezo wa hatua ya chama hicho kilichoianza Januari 24, mwaka huu jijini Dar es Salaam, kilipoandamana hadi katika ofisi za Umoja wa Mataifa kupeleka malalamiko yao.


Malalamiko hayo ni Serikali kutochukua hatua dhidi ya ugumu wa maisha kwa wananchi, Serikali isikilize maoni ya wananchi na iridhie kuanza mchakato wa mabadiliko ya Katiba.


Licha ya umati uliojitokeza kushiriki maandamano hayo yaliyohusisha safari ya kilomita 30.4 kutokea maeneo mbalimbali, baadaye mvua kubwa iliyonyesha ilikatisha hotuba za viongozi zilizopangwa kutolewa katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa.


Katika mkutano huo ulioanza saa 10:05 jioni, ni viongozi wanne pekee ndio walipata nafasi ya kuhutubia Taifa, huku viongozi wa kitaifa, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, John Mnyika na Makamu Mwenyekiti Bara, Tundu Lissu wakikosa nafasi hiyo kutokana na mvua kubwa.


Ilivyokuwa Katika maandamano hayo, viongozi wa kitaifa wa chama hicho waligawanyika katika maeneo matatu.


Mbowe alianzia Mbalizi, Lissu akitokea Uyole, huku Mnyika akianzia Isanga na makutano ya wote yalikuwa katika Uwanja wa Ruanda Nzovwe.


Safari ya Mbowe kutokea Uyole hadi katika makutano yaliyopangwa, ilikuwa na umbali wa takriban kilomita 18, Lissu kilomita nane na Mnyika ni Kilomita 4.5, zote zikijumuisha safari ya kilomita 30.4 ya maandamano katika Mkoa huo.


Katika maeneo yote wananchi walionekana kuitikia kwa wingi, huku Jeshi la Polisi likionyesha ushirikiano kama ilivyokuwa katika maandamano ya Dar es Salaam. Katika hali isiyotabirika, msafara wa Lissu ulikutana na msafara wa Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko.


Kukutana kwa misafara hiyo kulizua mzozo kati ya waandamanaji na Jeshi la Polisi, likiongozwa na Kamanda wake, Benjamin Kuzaga.


Baada ya mzozo huo uliodumu kwa takribani dakika nne, Jeshi la Polisi lilitumia busara na kupisha kwa kutumia njia ya mchepuko na kuondosha msafara wa Dk Biteko.


Hotuba Kwa upande wa Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema aliyejitambulisha kuwa Kiongozi wa Taasisi ya Sauti ya Watanzania, Dk Willibrod Slaa alitumia dakika tano za hotuba yake kujenga hoja mbili.


Moja ya hoja zake hizo ni kuweka sawa tafsiri ya taasisi hiyo ya Sauti ya Watanzania, akisema si chama cha siasa kama inavyopotoshwa na wengi, bali ni watu waliojiunga kushinikiza mabadiliko katika Taifa.


“Tunapambana na Serikali dhidi ya gharama za maisha, tunapambana na Serikali kupata Katiba mpya ili tufanye uchaguzi vizuri,” alisema Slaa.


Hoja ya pili ya mwanasiasa huyo aliyewahi kutangaza kukacha siasa za ndani ya vyama, ilikuwa ni kile alichokisema Rais Samia Suluhu Hassan hapaswi kuwaeleza wananchi kwamba muda uliobaki hautoshi kufanya mabadiliko ya Katiba.


Hoja yake hiyo, aliijenga kwa madai kwamba, Katiba iliyopo ilitengenezwa na watu wasiozidi 20 na kwa siku chache, hivyo inawezekana kuifanyia mabadiliko kwa muda mchache.


Alilisisitiza hilo kwa kueleza Rais Samia ni mwajiriwa wa Watanzania, hivyo wananchi ndio wanaopaswa kumwandikia mkataba wa ajira.


“Tunaungana na Chadema kwa nguvu zote na tutaungana na asasi na wale wote wanaopigania kupunguza gharama za maisha na wale wote wanaopambana tupate Katiba mpya,” alisema Slaa.


Hotuba ya Dk Slaa ilifuatiwa na Wakili Boniface Mwabukusi, aliyetumia takriban dakika saba, akidokeza kuendelea kwa kesi dhidi ya mkataba wa uendelezaji na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kati ya Serikali na DP World.


Katika kauli yake hiyo, Mwabukusi alisema pamoja na uamuzi wa awali wa Mahakama ya Mkoa wa Mbeya kuhusu shauri la mkataba huo, wanatarajia kwenda katika Mahakama ya Rufaa kuendelea na kesi hiyo.


“Kuna watu wanasema suala la bandari limekwisha tunawaambia hivi, tulishasema na tunarudia tena. Bandari ni urithi wetu, haitauzwa kamwe wala hautakwenda kwenye mikono ya mgeni,” alisema Mwabukusi.


“Mungu anapoumba eneo lolote anakupa ardhi, mbingu yako na mipaka yako ambayo haiwezi kugawanyika au kuwekwa kwenye mikono ya wageni.” Alieleza Serikali ya Tanzania inakabidhi rasilimali za asili kwa mikataba isiyofaa.


“Kwa hili tuna wajibu wa kuomba radhi kwa Watanzania wote kwa aibu tuliyoisababisha,” alisema.


Kuhusu sababu za kuiunga mkono Chadema, alisema: “Mungu huwa anainua chama, anainua watu, anainua taasisi kusimama kwa ajili yake, hakuna mahali utamuona Mungu akitembea, tunaiunga mkono Chadema.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad