Tuzo za 66 za Grammy zinafanyika Jumapili kwenye ukumbi wa Crypto.com mjini Los Angeles, California, Marekani, ambapo wanawake walitarajiwa kufanya vyema zaidi kuliko wanaume katika nafasi mbalimbali, kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya burudani.
Mtayarishaji mkuu wa Grammys Ben Winston alisema awali kwamba wanawake wangetawala katika tamasha za mwaka huu ambazo zilianza mwendo wa saa mbili usiku saa za Washington.
Hafla hiyo ilipeperushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha CBS, ikiongozwa na Mchekeshaji Trevor Noah, ambaye alifanya hivyo kwa mwaka wa nne mfululizo.
Tofauti na tamasha zingine, Grammys huwashirikisha wasanii mbalimbali kote duniani.
Kwa mara ya kwanza mwaka huu kuna tuzo jipya la onyesho bora la muziki wa Kiafrika, tuzo ambayo inaashiria umaarufu unaoongezeka wa mtindo wa Afrobeats, na aina nyingine ya muziki kutoka kwa bara hilo, ambao uanaendelea kupata umaarufu kimataifa kupitia majukwaa ya mitandao ya kijamii kama vile TikTok.
Asili ya Afrobeat ni ukanda wa Afrika Magharibi, hasa Ghana na Nigeria, ingawa neno hilo mara nyingi hutumika kama mvuto kwa mitindo mbalimbali ya muziki inayotoka Afrika.
Mwanamuziki raia wa Nigeria Burna Boy, ni kati ya waliokuwa na matarajio ya kuibuka washindi katika tamasha hilo, na pia alikuwa mmoja wa watumbuizaji.