Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga amesema kutokana na jitihada za Serikali na wakandarasi, kwa mara ya kwanza jana Februari 15, 2024 yamefanyika majaribio ya kuwasha mtambo namba tisa wa kufua umeme katika Bwawa la Julius Nyerere na inategemea kuuzindua mtambo huo mwezi huu.
Kapinga ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Lupembe, Edwin Swalle aliyetaka kujua ni ipi kauli ya Serikali kwa kuwa kumekuwa na taarifa mitandaoni kuwa mitambo miwili ya kufua umeme katika bwawa hilo ingezinduliwa leo Februari 16,2024.
Amesema katika majaribio ya mtambo huo, Serikali imeutembeza hadi kufikia uwezo wake wa mwisho wa kuzalisha megawati 235 za umeme.
Naibu Waziri Kapinga amelihakikishia bunge kuwa mpango wa kuuzindua mtambo huo mwezi huu wa Februari uko palepale ambapo kwa sasa wataalamu wanaendelea kukamilisha hatua za mwisho ikiwa ni pamoja na kuimariaha ulinzi wa mtambo kwa ajili ya kuendelea na ratiba za uzalishaji umeme nchini.