Kiungo aliye katika ubora wa juu, Feisal Salum, amezidi kumkaribia kinara wa mabao Stephane Aziz Ki wa Yanga baada ya kufunga bao lililoiwezesha Azam FC kupata sare ya 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Fei alifunga bao hilo kwa njia ya penalti na kuisawazishia Azam katika dakika ya 54 baada ya beki na nahodha wa Prisons, Jumanne Elfadhil kuunawa mpira eneo la hatari na mwamuzi Ally Mnyupe wa Morogoro kuamuru adhabu hiyo.
Hilo lilikuwa ni bao la tisa kwa Fei na kumkaribia zaidi kiungo wa Yanga, Aziz Ki mwenye mabao 10 katika mbio za kuwania tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu Bara.
Tangu ameanza kucheza Ligi Kuu Bara akiwa na Yanga mwaka 2018, Fei hakuwahi kufunga mabao zaidi ya sita kwenye michuano hiyo, lakini baada ya kujiunga na Azam katika uhamisho uliojaa utata hadi kuombewa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ‘aachiwe aende atakako’, nyota huyo maarufu kama ‘Zanzibar Finest amekuwa katika ubora wa juu kabisa mbele ya lango.
Kiwango chake kimeiwezesha Azam kuwa timu inayoongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu Bara kufikia sasa raundi ya 17 ya mechi, ikiwa imepachika mabao 39 sawa na vinara Yanga ambao hata hivyo wana mechi moja mkononi kwani wamecheza mechi 16. Hata hivyo, Azam imeruhusu mabao 13, wakati Yanga imeruhusu mabao manane tu, ikiwa timu iliyofungwa mabao machache zaidi kufikia sasa.
Sare imeibakisha Azam katika nafasi ya pili ya msimamo ikiwa na pointi 37, pointi sita nyuma ya Yanga yenye pointi 43. Simba iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 36 ikiwa imecheza mechi 15, mbili pungufu ya ilizocheza Azam.
Prisons ilitangulia kupata bao kupitia kwa straika Samson Mbangula aliyeunganisha vyema pasi ya mkongwe Benjamin Asukile na kwenda mapumziko wakiwa mbele.
Pamoja na kutanguliwa kufungwa Azam haikuwa kinyonge kutokana na mashambulizi iliyofanya japokuwa hatari zao ziliishia mikononi mwa kipa wa Prisons, Yona Amos huku nyingine zikipaa nje ya lango.
Kabla ya mchezo huo, Prisons ilikuwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Singida Fountain Gate huku Azam ikitoshana nguvu ya bila kufungana na Tabora United.
Azam ilihitaji kuendeleza ubabe na rekodi kwa Wajelajela hao baada ya mchezo wa mzunguko wa kwanza kuishindilia Prisons mabao 3-1 zilipokutana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam na kujikuta leo wakichezeshwa kwata na kuondoka na sare hiyo.
Azam inafikisha sare ya tatu katika mechi nne nyuma za Ligi Kuu ikianza dhidi ya Simba 1-1, suluhu mbele ya Tabora United na leo dhidi ya Maafande hao, kabla ya kuilaza Geita Gold 2-1 michezo yote ikiwa ugenini. Hapo kati pia iliichakaza Green Warriors 5-0 katika mechi ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
Timu zote zilifanya mabadiliko Azam iliwapumzisha Lusajo Mwaikenda, Feisal Salum, Adolf Bitegeko na Abdul Suleiman ‘Sopu’ na nafasi zao kuingia Idd Nado, Kipre Juniors, Nathan Chilambo na Ayoub Lyanga na kufanya timu hiyo kuonekana kuchangamka zaidi.
Kwa upande wa Prisons waliwapumzisha Asukile, Zabona Hamis, Ally Msengi huku Joshua Nyatin, Salum Kimenya na Benedict Jacob wakiingia kuziba nafasi hizo ambapo timu zote hazikuweza kubadili matokeo kwa dakika 90.
Mbangula anakuwa mchezaji aliyefunga kwenye mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu akianza na mchezo uliopita dhidi ya Singida FG na kufikisha mabao manne.