Walichozumgumza Rais Samia na Papa Huko Vatican



Dar es Salaam. Katika kujenga na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican, leo Februari 12, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.

Kwa mujibu wa tovuti ya Vatican, katika mazungumzo ya faragha yaliyodumu kwa takribani dakika 25, wameeleza kuridhishwa na uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Vatican na Tanzania.

Pia wamezungumzia mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi na maendeleo kwenye sekta za elimu, afya na ustawi wa jamii.

Mbali ya hayo, wamezungumzia changamoto ambazo Tanzania inapitia kwa sasa.

Viongozi hao wamezungumzia masuala ya kijamii, kikanda na kimataifa, ikiwamo umuhimu wa jumuiya ya kimataifa kujikita katika kudumisha amani duniani.

Rais Samia pia amekutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa.

Rais Samia katika ziara hii ya kitaifa, ameambatana na Evaline Ntenga, ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa WUCWO Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (Wawata) Taifa nchini Tanzania.

Wengine ni Profesa Deogratias Rutatora, ambaye ni Mwenyekiti Halmashauri ya walei, Taifa; Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania, Taifa, (Viwawa), Dalmas Gregory, Mwenyekiti Halmashauri Walei, Jimbo Katoliki la Zanzibar na Theresia Seda, Mwenyekiti wa Utoto Mtakatifu, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.


Ziara hiyo inalenga kukuza uhusiano wa kidiplomasia baina ya Vatican na Tanzania ambao ulianza miaka ya 1960, Vatican ilipoanzisha ubalozi nchini.

Kanisa Katoliki limekuwa likichangia kwa kiasi kikubwa kabla na baada ya uhuru wa Tanzania Bara kwa kutoa elimu kwa Watanzania. Linakadiriwa kumiliki zaidi ya shule za awali 240, shule za msingi 147, za sekondari 245, vyuo vya ufundi 110, na vyuo vikuu vitano.

Kupitia shule na vyuo hivyo, kanisa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania limechangia kuzalisha viongozi na wataalamu mahiri kwenye maeneo mbalimbali.

Kwenye sekta ya afya, Vatican kupitia kanisa imeendelea kutoa huduma bora za afya kwa Watanzania, ikikadiriwa hadi sasa kuendesha takriban taasisi za afya 473.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad