Wasiopita JKT, JKU kuajiriwa vyombo vya usalama

Wasiopita JKT, JKU kuajiriwa vyombo vya usalama


Bunge limeazimia kwamba vijana wote wapewe fursa sawa katika ajira pale ambapo wanakuwa wametimiza masharti mengine yote yanayohusika na nafasi husika isipokuwa cheti cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) hadi pale ambapo Serikali itakapokuwa na uwezo wa kuwapokea na kuwapa mafunzo ya JKT na JKU Vijana wote wanaohitimu kidato cha nne na cha sita.


Azimio hilo limepitishwa kufuatia mjadala uliokuwa ukiendelea bungeni jijini Dodoma juu ya hoja ya dharura iliyotolewa na Mbunge wa jimbo la Mbozi, George Mwenisongole hapo jana iliyetaka Bunge kuielekeza Serikali kutotumia kigezo cha kupitia mafunzo ya JKT katika kuajiri vijana katika vyombo vya ulinzi na usalama.


Hoja hiyo ilipowasilishwa hapo jana haikupata nafasi ya kujadiliwa bungeni kwa kile kilichoelezwa kuwa hadi Spika wa Bunge atakapojiridhisha kupitia taarifa rasmi za kumbukumbu za bunge [hansard] kuwa hapo awali Bunge lilitoa maazimio gani kuhusu suala hilo.


Baada ya kujiridhisha na taarifa rasmi za kumbukumbu ya Bunge Spika Tulia amebaini kuwa suala hilo halikuazimiwa japokuwa kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo ambacho ni 2021 hadi 2024 jambo hilo limekuwa likiibuliwa bungeni kama ushauri.


Hivyo Spika alimruhusu mtoa hoja kutoa hoja hiyo bungeni kwa ajili ya wabunge kuchangia na baada ya michango hiyo ndipo akatangaza kuwa Bunge limeazimia kwamba kigezo cha kijana kupita JKT na JKU ndio awe na sifa za kuajiriwa katika vyombo vya ulinzi na usalama kiondolewe.


Azimio hilo halitahusisha mchakato wa ajira ambao umekwishafanyika isipokuwa kwa ajira zinazokuja kuanzia sasa.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad