Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za mauaji ya Mohamed Ameir (35), mkazi wa Magomeni- Mwembechai wilayani Kinondoni.
Taarifa iliyotolewa jana Februari 2, 2024 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro inaeleza mwili wa Ameir umekutwa katika fukwe za Kigamboni, Februari mosi, 2024.
“Taarifa za awali zilipatikana kwa Jeshi la Polisi kutoka kwa ndugu wa marehemu kuwa Januari 28, 2024 mtu huyu hakuonekana na baadaye ikadaiwa alitekwa na watu waliotaka kupewa fedha Sh3 milioni.
“Jeshi la Polisi linafanya mahojiano ya kina kwa watuhumiwa hao wawili, jitihada zinafanyika ili kuhakikisha wengine nao wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi,” amesema Kamanda Muliro bila kuwataja watuhumiwa hao.
Tukio hilo limekuja wakati kukiwa na taarifa za watu kutoweka na kutekwa maeneo mbalimbali nchini.
Miongoni mwa matukio hayo ni la kutekwa kwa aliyekuwa mfanyabiasha na fundi simu eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, Innocent Elias Liveti (34) maarufu Macheni.
Kwa mujibu wa mashuhuda na picha za video zilizochukuliwa na kamera za usalama (CCTV), siku hiyo Desemba miso, 2023 saa 1:30 asubuhi Liveti alikuwa amekaa mbele ya duka lake lililopo Mtaa wa Narung'ombe, walitokea watu wawili waliovalia kofia, walimchukua na kuingia naye ndani ya gari na kuondoka naye.
Tukio lingine ni la kutekwa kwa mfanyabiashara, Mussa Mziba (37) aliyekuwa akimiliki kampuni ya Mziba Empire Investment Ltd yenye ofisi zake Mikocheni, Dar es Salaam.
Mziba alidaiwa kutekwa na watu wawili waliofika ofisini kwake saa 2 usiku, Desemba 7, 2023 wakijitambulisha kuwa ni maofisa wa polisi.
Matukio hayo yametanguliwa na kutoweka kwa Charles Wetinyi, aliyedaiwa kukamatwa na watu waliojitambulisha kuwa polisi, eneo la Mugumu wilayani Serengeti Mkoa wa Mara Oktoba 23, 2023.