Waziri Masauni Ataja Chanzo vya Watu Kutekwa, Kupotea



Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni ametaja vyanzo vya matukio ya utekaji na kupotea kwa watu kuwa ni wivu wa mapenzi, ushirikina, kugombania ardhi, urithi, kujiteka, visasi na utapeli.

Kauli ya Waziri Masauni imekuja wakati matukio ya watu kupotea yakishika kasi nchini, huku ikielezwa kuwa baadhi ya matukio hayo yanahusishwa na watu waliohusika katika matukio ya uhalifu.

Akichangia katika taarifa ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa mwaka 2023 jana Ijumaa Februari 9, 2024, Waziri Masauni amesema hoja ya wananchi kutekwa inaweza kutoa taswira kama labda kuna tatizo kubwa sana na kuzua taharuki kubwa katika jamii.

Amesema kwa takwimu alizonazo kuanzia Januari hadi Desemba mwaka 2023, asilimia 72.5 ya watu waliopotea walishapatikana.

“Sio kwamba watu wanapotea hakuna kilichofanyika Polisi hawawapati wahalifu wahanga sio sahihi, kuna kazi kubwa imefanyika na matunda yake ni hayo niliyozungumza.”

“Vyanzo vilivyobainika ni wivu wa mapenzi, ushirikina, kugombania ardhi, mpaka kujiteka ipo, visasi, utapeli, asilimia kubwa ya vyanzo ni mambo haya,” amesema.


View this post on Instagram
A post shared by Mwananchi (@mwananchi_official)

Kauli Waziri Masauni ilikuja muda mfupi baada ya Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima kusema kuwa wiki mbili zilizopita mtoto wa Mohamad Alli Jabiri alitekwa Dar es Salaam na maiti yake ikaja kuokotwa baadaye ikiwa imekatwa vipandevipande na macho yametobolewa.

Gwajima amesema Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda anayezunguka katika ziara ya kukijenga chama, kila mahali anapofika wananchi wanampa taarifa za kupotea, kutekwa, kutoonekana na kutopatikana kwa watu.

“Kiongozi huyu anapokea sana malalamiko ya watu hawa… Naomba waziri kulitolea ufafanuzi jambo hili ili kuondoa sintofahamu ya kuichafua Serikali yetu njema ya Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.

Akiendelea kufafanua, Waziri Masauni amesema madhumuni ya kuwa na vyombo vya dola ni kuzuia uhalifu na Tanzania imebahatika kuwa navyo imara vinavyoheshimika na kusifika.

Amesema wabunge ni mashahidi kuna wakati kulitokea wimbi la uhalifu, kudhuru albino, uhalifu wa Kibiti mkoani Pwani, panya road ambayo yote yalidhibitiwa na Jeshi la Polisi na hali ilitulia.

“Tuwe na imani na vyombo vyetu vya usalama hasa Jeshi la Polisi. Ni makosa sana kutengeneza taswira ya kuondoa imani ya chombo cha usalama kama Jeshi la Polisi ambalo linafanya kazi kubwa mbele ya jamii,” amesema.

Amesema mambo yote yahitaji elimu na ndio maana wameshusha Polisi jamii hadi katika ngazi ya kata ili wananchi wapate uelewa.

Amewataka watu wasioridhika na uchunguzi wa Jeshi la Polisi kuhusiana na matukio hayo, kuwasilisha malalamiko yao wizarani.

Masauni amesema yeye amepokea malalamiko manne na kuyaundia tume ambayo imewashirikisha watu kutoka taasisi mbalimbali za umma.

Hata hivyo, amesema masuala ya uchunguzi yanahitaji muda na kwamba mtu yoyote anaweza kusema, lakini kufanya hivyo hakuna maana kuwa halijafanyiwa kazi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad