Waziri Nape Aingilia Kati Sakata la Lissu Kuzuiwa Mahojiano Wasafi FM 'Wasafi Kuweni Wakweli'




Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nauye amesema hakukuwepo na "maagizo yoyote kutoka juu" katika kuzuia mahojiano ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu na kipindi cha Good Morning cha Wasafi TV .

Hivyo, Waziri Nape amevitaka vyombo vya habari nchini kutoa uwanja sawa kwa wanasiasa huku akiwaonya wanaotaka kuzuia baadhi ya watu akisema hiyo ni njia ya kumhujumu Rais Samia Suluhu Hassan.

Nape ametoa kauli hiyo leo Februari 7, 2024 jijini Dodoma saa chache baada ya mahojiano ya yaliyoandaliwa na Wasafi TV na Lissu kuahirishwa, lakini mwanasiasa huyo akaamua kufuatilia kwenye chombo hicho kujua nini kimetokea.

“Vyombo vyote habari, wapeni wanasiasa uwanja sawa watimize majukumu yao, mtu akisemwa, wa upande wa pili apewe nafasi, ndio namna ya kuendesha siasa za nchi yetu,” ameelekeza Nape.

Nape amesema amesikitishwa na madai dhidi ya Serikali yaliyoenea kufuatia kufutwa kwa mahojiano hayo, ikidaiwa kuwa "ni maagizokutoka juu."

“Maneno kwamba kuna maagizo kutoka juu, limetusikitisha. Nimekuja kuwathibitishia msimamo wa Rais katika kuimarisha uhuru wa wanahabari na demokrasia katika nchi yetu kwamba uko palepale.

“Serikali haijafanya na haina mpango wa kuingilia vyombo vya habari,” amesema.

Nape amewataka wanahabari kutokuwa na hofu na visingizio kwamba kuna maagizo.

Amesema wanahabari wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa kufuata sheria na Serikali haitaingilia uhuru wao katika kutimiza majukumu yao.

Mapema leo Februari 7, 2024 Lissu alifika ofisi za Wasafi TV kuhoji sababu za kuahirishwa kwa mahojiano naye, ambayo tayari yalikuwa yametangazwa kuanzia jana na kwenye mitandao ya kijamii.

Baadaye Lissu amesema matatizo ya mawasiliano miongoni mwa waandaaji wa kipindi cha Good Morning na menejimenti ya Wasafi TV ndiyo sababu ya kuahirishwa kwa mahojiano hayo leo.


Hata hivyo, Lissu amesema alipopata mwaliko huo alipata wasiwasi kwa sababu kumekuwa na matatizo kwenye vyombo vya habari kwa miaka kadhaa.

"Nilikuwa na shaka kwamba kweli mamlaka itakubali mimi nije kwenye kipindi hiki, lakini baadaye walinitoa shaka kwamba wamezungumza na wakuu wao na kwamba kila kitu kiko sawa," amesema Lissu.


Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akiwa kwenye Ofisi za Wasafi TV alipoenda kuhoji nani ametoa maelekezo kuahirisha mahoajino naye leo Februari 7, 2024.
Lissu amesema jana jioni alipokea habari kwamba kipindi kimeahirishwa, na alipohoji aliambiwa ni maagizo kutoka juu, jambo ambalo hata hivyo, viongozi wa chombo hicho wamesema si kweli.

Katika mazungumzo yake na viongozi wa chombo hicho, Lissu amesema wamemhakikishia kwamba kipindi hakikuahirishwa kwa sababu ya maagizo kutoka juu, bali kulikuwa na matatizo ya mawasiliano miongoni mwa waandaaji wa kipindi na menejimenti, jambo ambalo lingesababisha kipindi kutokuwa bora.

"Sina sababu ya kutokuamini maneno yao, tumekubaliana kwamba tutafute muda wafanye maandalizi yanayostahili ili nije kufanya kipindi katika siku zijazo," ameongeza Lissu.

Mwananchi inaendelea na juhudi za kuupata uongozi wa Wasafi TV ili kuzungumzia kilichotokea hadi kuahirishwa kwa mahojiano hayo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad