Yanga Waitandika Mashujaa, Mudathir Aendelea kutawala Chamazi

 

Yanga Waitandika Mashujaa, Mudathir Aendelea kutawala Chamazi



Vichwa vya habari vya Mudathir Yahya kuing’arisha Yanga ichezapo kwenye Uwanja wa Azam Complex inaonekana vitaendelea baada ya jana tena kufunga bao la ushindi wa 2-1 dhidi ya Mashujaa katika mechi ngumu ya Ligi Kuu Bara.


Bao hilo limekuja siku tatu tu tangu alipofunga bao jingine la ushindi wa 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji katika mechi nyingine ambayo Yanga ilikuwa ikionekana kuelekea kudondosha pointi na kumfanya staa huyo zamani wa Azam FC kujitangazia ufalme wa uwanja huo aliolelewa.


Yanga imeendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kukusanya pointi 37 baada ya mechi 14, ikiwa inaendelea kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.


Timu hiyo ilianza kujipatia bao kupitia kwa Maxi Nzengeli katika dakika ya 45, ambaye alikuwa hajafunga kwenye michezo 10 mfululizo, tangu alipofanya hivyo kwenye ushindi wa 5-1 dhidi ya Simba kwenye Dabi ya Kariakoo mwaka jana. Sasa Maxi amefikisha mabao manane sawa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam na Jean Baleke aliyekuwa akiitumikia Simba kabla ya kutemwa katika dirisha dogo la usajili lililopita Desemba mwaka jana.


Mudathir aliendelea kuonyesha umwamba wake baada ya kuifungia Yanga bao la ushindi katika dakika ya 86 akimalizia krosi ya Kennedy Musonda, likiwa ni bao lake la pili la ushindi anafunga kwenye michezo miwili mfululizo baada ya kufanya hivyo kwenye dakika za mwisho pia kwenye mechi dhidi ya Dodoma Jiji.


Mashujaa Dakika 45 bila shuti


Ndani ya dakika 45 za kwanza Yanga ilipata shida kuupangua ukuta wa Mashujaa iliyocheza kwa kujilinda zaidi mbinu ambayo iliwaweka wenyeji kwenye wakati mgumu kukamilisha mashambulizi yao licha ya kuwaandama wageni hao huku kipa wao Eric Johora, ambaye amewahi kudakia Yanga, akiokoa kishujaa hatari zote za mapema.


Mashujaa haikufanya shambulizi la maana ndani ya dakika 45 za kwanza ambapo haikupiga shuti lolote sio la kulenga lango wala lililoenda nje la lango wakati Yanga ikipiga mashuti 7 yaliyolenga lango.


Guede mambo bado


Mshambuliaji mpya Joseph Guede amecheza mchezo wake wa tatu akiwa na Yanga akipewa zaidi ya dakika 131 baada ya jana kucheza dakika 86 bila kupata bao lolote akipiga mashuti mawili pekee yaliyolenga lango.


Guede bado anaendelea kuonyesha ubora wa kuwachezesha wenzake kuliko kushambulia kwa kufunga huku akikosa utulivu wa kukaa sana ndani ya eneo la hatari huku muda mwingi akionekana kutohusika katika mchezo, jambo ambalo liliifanya Yanga ionekane kama inacheza na watu 10 uwanjani.


Bao la nne ugenini Mashujaa


Mashujaa ilizinduka kipindi cha pili kuanzia dakika 60, ilipofanya mabadiliko manne kwa pamoja ikiwatoa Omari Omari, Zuberi Dabi, Reliant Lusajo na Jermanus Josephat nafasi zao zikichukuliwa na Mapinduzi Balama, Emmanuel Mtumbuka na Hassan Ally.


Mabadiliko hayo yaliiwabeba Mashujaa ilifanikiwa kupata bao lao la nne katika mechi za ugenini msimu huu mfungaji akiwa Emmanuel Mtumbuka Mtumbuka katika dakika ya 66, akimchungulia kwa mbali kipa wa Yanga Aboutwalib Mshery.


Baada ya bao hilo Mashujaa ilibadilika na kuendelea kufanya mashambulizi kwenye lango la Yanga ilifanikiwa kupiga jumla mashuti matatu kipindi cha pili huku moja likizalilisha bao hilo lao la kufuatia machozi.


Ufunguo wa ngome


Mapumziko marefu ya kupisha Kombe la Mapinduzi na fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, yanaonekana kuiathiri Yanga ambayo imepoteza wepesi wake katika kuwamaliza wapinzani na hivyo kujikuta ikipata matokeo ya taabu ikitoka 0-0 dhidi ya Kagera Sugar, ikishinda 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji na ushindi wa wa 2-1 dhidiu ya Mashujaa.


Kukosekana kwa kinara wake wa mabao Aziz Ki kunaonekana kuchangia Yanga kukosa ufunguo wa ngome za wapinzani.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad