Yanga Wavuna BIL 2.3 za CAF, Pacome, Aziz Ki Walamba Milioni 400....Hesabu Zote Hizi Hapa

Yanga Wavuna BIL 2.3 za CAF, Pacome, Aziz Ki Walamba Milioni 400....Hesabu Zote Hizi Hapa


Yanga imejihakikishia kuvuna Dola 900,000 (zaidi ya Sh2.3 bilioni) kwa kutinga robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika jana Februari 23, 2024.

Mabingwa hao wa Tanzania wamefuzu hatua hiyo baada ya kuichapa CR Belouizdad mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Yanga ilifuta gundu la miaka 25 baada ya kutinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika na kuvuna Sh1.8 bilioni Septemba 30, 2023 ilipoing’oa Al Merrikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-0.

Endapo Yanga itafanikiwa kutinga nusu fainali ya mashindano hayo itavuna kitita cha Sh3.1 bilioni huku mshindi wa pili atapata Sh5.1 bilioni

Bingwa wa michuano hiyo atavuna zaidi ya Sh10.2 bilioni kiasi ambacho walipata Al Ahly msimu uliopita baada ya kuichapa Wydad 3-2 kwenye fainali hizo.

Yanga imeitangulia Simba kufuzu robo fainali na kuungana na bingwa mtetezi Al Ahly, Mamelodi Sundowns, TP Mazembe, Petro Luanda na Asec Mimosas.

PACOME, AZIZ KI WALAMBA MIL 400.

Mashabiki wa Yanga bado wako kwenye sherehe ya ushindi mkubwa dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria na kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa na mchezo mmoja mkononi, lakini kocha wa timu hiyo Miguel Gamondi amesema kazi haijaisha, huku mastaa wa timu hiyo wakivuna Sh400 milioni za ushindi huo wa kibabe.

Yanga imesaliwa na mechi mechi dhidi ya vinara wa sasa wa kundi D na watetezi wa taji, Al Ahly ya Misri mechi itakayopigwa Ijumaa hii na kocha Gamondi ameweka wazi kuwa ‘haijaisha hadi iishe’ wakitaka ushindi ugenini kusudi aongoze kundi hilo ili iwe na kazi rahisi kwenye robo fainali ambayo droo yake inatarajiwa kufanyika mwezi ujao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema amefurahia timu hiyo kujihakikishia nafasi ya kucheza robo fainali baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Belouizdad lakini hapo hapo bado anafikiria kwenda Misri kuwafuata Al Ahly akitaka kusaka ushindi.

Gamondi alisema anajua kuna faida kubwa, Yanga ikimaliza kinara wa Kundi D ambapo haitakuwa na ugumu mkubwa kuelekea droo ya nani wakutane naye kwenye hatua ya robo fainali, lakini akiwakumbusha mastaa wake kuwa makini kuzitumia nafasi inazotengeneza ili kupata mabao mengi, kwani hata juzi ilistahili kushinda kwa idadi kubwa zaidi.

“Kwangu hatua ya kufuzu kwenda robo fainali nimeridhika, lakini ukweli ni kwamba kuna faida kubwa kama tukimaliza vinara wa kundi letu mbele ya Al Ahly. Safu ya ushambuliaji ina udhaifu, inatengeneza nafasi nyingi inatumia chache pia eneo la ulinzi kuna makosa madogo madogo nikifanikiwa kurekebisha na wakinielewa Yanga itakuwa timu bora Afrika kwa ushindani,” alisema Gamondi na kuongeza;

“Mimi ni kocha ninayependa kushinda wakati wote, kila mtu anajua namna ambavyo tulipambana na Ahly hapa, ni klabu kubwa na bora lakini kila kitu kinawezekana tutakwenda kujaribu kwenda kucheza kwa akili kubwa tutafute ushindi hukohuko kwao (Ahly).”

Matokeo ya juzi katika pambano hilo lililopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam yamewapa nyota wa timu hiyo wakiongozwa na aliyekuwa na shughuli yake, Pacome Zouzoua, Stephane Aziz KI, Djigui Diarra na Mudathir Yahya zaidi ya Sh 400 milioni kutoka kwa mabosi wa klabu hiyo.

Ipo hivi. Kabla ya mchezo huo mabosi wa Yanga wakiongozwa na mfadhili wao Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ walifanya kikao flani cha mtego wa mamilioni kwa wachezaji wao. Mtego wenyewe ulikuwa hivi mabosi wa Yanga waliwaambia wachezaji wao kwamba kama wakishinda bao moja hadi mawili, basi wangevuna Sh100 milioni pekee, lakini kama ingeshinda mabao 3-0 basi dau lingeongezeka hadi Sh200 milioni, lakini kama itavuka malengo kwa kushinda mabao 4-0 watajihakikishia Sh400 milioni kwa ushindi huo.

Kama uliona juzi wachezaji wa Yanga walipofunga bao la nne tu wale waliokuwa benchi na hata wale baadhi ya waliokuwa uwanjani walionyesha vidole vinne eneo la Jukwaa Kuu wakiwakumbusha viongozi wao kwamba nne zimetimia.

Mbali na fedha hizo, Yanga imevuna Sh20 milioni kutoka kwenye ahadi ya Rais Samia Hassan.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad