Mfanyabiashara Ramadhani Ntuzwe ‘Babu Rama’ aliyekuwa akipaza sauti katika vyombo mbalimbali vya habari kwa takribani miaka saba kwamba anaidai fidia ya Sh 987 milioni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), anadaiwa kujiua kwa risasi leo Jumatano dukani kwake Urambo mkoani Tabora.
Meneja wa mfanyabiashara huyo, Msifuni Myava amethibitisha kutokea kwa kifo cha bosi wake na kudai kuwa amejipiga risasi ya kichwa na kupoteza maisha akiwa amejifungia dukani kwake.
Pia, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuueleza mtandao wa MwanaHALISI kuwa taarifa kamili kuhusu kifo cha mfanyabiashara huyo atazitoa baadae.
Hata hivyo, Meneja huyo amesema Mfanyabiashara huyo alikuwa amepatwa msongo wa mawazo kwa muda mrefu tangu alipodaiwa kunyang’anywa jumba lake katika eneo la Kariakoo.
Amesema hali hiyo ilisababisha Ramadhan Ntuzwe kujifungia ndani muda mwingi. Akisimulia mkasa huo amesema, leo asubuhi kulitokea msiba wa kaka wa mfanyabiashara huyo hivyo mdogo wao akaenda dukani kwa Ramadhani kumpa taarifa kuwa kaka yao mkubwa amefariki kisha akaondoka.
“Sasa aliporudi kuja kumuuliza wanafanyaje kuhusu taratibu za mazishi ya kaka yao mkubwa, akakuta mlango umefungwa kwa ndani, alipoita majirani na kuuvunja wakakuta Ramadhani Ntuzwe naye amefariki kwa kujipiga risasi,” amesema Myava.
Mfanyabiashara huyo kwa mara ya kwanza aliwasilisha kilio chake tarehe 28 Februari 2019 katika kikao cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na wafanyabiashara wa Ilala ikiwa ni miezi saba tangu alipokutana na mkasa huo tarehe 30 Oktoba 2016 alipokuwa akisafirisha mzigo wake kutoka Afrika Kusini kupitia mpaka wa Tunduma kuelekea Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, Ntunzwe alieleza mikasa miwili iliyomkuta dhidi ya TRA; kwanza kushikilia mzigo wake kwa miaka mitatu kwa tuhuma za kukwepa kukodi huku yeye akidai kukataa kutoa rushwa ya Sh2milioni na mkasa wa pili ni kuibiwa mali zake zenye thamani ya Sh986 milioni katika duka lililopo Kariakoo baada ya TRA kulifunga kwa madai ya kutotumia mashine ya EFD.