Ukisikia mechi dume ndo hii. Ni mechi ya lawama vilevile. Lakini kama utapenda kuiita mechi ya kibingwa pia hautakosea, wakati watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, kesho Jumapili watakapokuwa wageni wa Azam FC kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Yanga ndio mabingwa waliotwaa mara nyingi taji la Ligi Kuu ikifanya hivyo mara 29, wakati Azam ni moja ya timu zilizotwaa mara moja msimu wa 2013-2014 na msimu huu imeonekana kupania licha ya kwamba katika mechi za karibuni ilidondosha pointi nyingine zilizowaengua kileleni mwa msimamo.
Kama hujui hii ni mechi pekee ya Ligi Kuu Bara inayopigwa Jumapili kwani hakuna mchezo wowote utakaopigwa, lakini leo Jumamosi itashuhudiwa mchezo mmoja Singida Fountain Gate na Namungo zinazoumana jioni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Mechi ya kesho itakuwa ni mechi ya mwisho ya Ligi Kuu kabla ya ligi hiyo haijasimama kupisha mechi za kimataifa kwa timu za taifa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na mashabiki wameitolea macho kutaka kujua nani ataibuka na ushindi baada ya kelele na tambo nyingi nje ya uwanja.
Kwa namna ratiba ilivyowekwa ni kama vile leo mashabiki wa soka wameachiwa muda wa kuijadili mechi hiyo ya 32 baina ya timu hizo kukutana katika Ligi Kuu tangu 2008 kabla ya kesho kuishuhudia mara baada ya watu kutoka kupata futari pamoja na chakula cha jioni.
Kwa wale ambao hawatabahatika kwenda Kwa Mkapa wataishia kukaa katika sebule zao au kuibukia vibanda umiza ili kushuhudia mtanange huo, ikizangitiwa kuwa Yanga na Azam haijawahi kuwa mechi ndogo.
Awali mechi hii ilikuwa ipigwe Uwanja wa Azam Complex, kuanzia saa 1:00 usiku, lakini ikahamishiwa Kwa Mkapa na kubadilishiwa muda vile vile hadi saa 2:30 usiku ili kuwapa wasaa mashabiki wanaoendelea na mfungo wa mwezi wa Ramadhani na Kwaresima kufuturu kabisa ndipo waibukue uwanjani kucheki shoo kali.
VITA TATU TOFAUTI
Mechi ya kesho imegawanyika katika maeneo matatu tofauti - kwanza upinzani na ushindani mkali uliopo baina ya timu hizo, lakini ni ya kutoa dira ya ubingwa kwa msimu huu, huku ikiwa mechi ya vita ya mastaa wa timu hizo wanaochuana kwenye kuwania tuzo mbalimbali za ligi hiyo.
Yanga inayoongoza msimamo kwa sasa ikiwa na pointi 52 itahitaji ushindi ili kuzidi kujikita kileleni na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutetea taji kwa msimu wa tatu mfululizo, lakini ikitaka kuendeleza ubabe dhidi ya Azam ambayo imeshind
a mara ya mwisho kwenye ligi mbele ya Yanga Aprili 25, 2021. Katika mechi hiyo pekee ya Azam kuifunga Yanga, bao liliwekwa kimiani na Prince Dube ambaye ameibua tafrani hivi karibuni kuigomea timu hiyo akilazimisha kuondoka, huku akihusishwa na Yanga.
Azam itashuka uwanjani kutaka kujivua joho la unyonge mbele ya Yanga, lakini ikisaka alama tatu kuzidi kuiweka pazuri katika msimamo na kuinasa tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu ujao ikichuana na Simba.Kabla ya mechi ya jana usiku kati ya Simba na Mashujaa, Wanalambalamba walikuwa nafasi ya pili na pointi 44 baada ya mechi 20, huku Simba ikiwa nyuma yao kwa tofauti ya alama mbili, kwani ilikuwa na 42 na kama imeshinda mchezo huo, basi ilikuwa na nafasi ya kuiengua Azam kwani ingefikisha pointi 45.
Kama itakuwa imeshushwa na Simba ni wazi, itataka kushinda mbele ya Yanga ili kurejea nafasi ya pili wakati ligi ikienda mapumziko na pia kupungua pengo la pointi kutoka nane zilizopo sasa hadi kuwa tano, licha ya kuwa na mchezo mmoja mbele zaidi ya wapinzani wao. Azam imecheza mechi 20 na Yanga 19.
SHOO YA KIBABE
Mbali na vita ya pointi za ubingwa, lakini mechi ya kesho ni shoo ya mastaa ambao msimu huu wamekuwa tishio katika Ligi Kuu.
Yanga inatambia Pacome Zouzoua, Stephane Aziz KI, Maxi Nzengeli, Kenendy Musonda, Yao Kouassi, kipa Diarra Djigui, Ibrahim Bacca na wengineo ambao katika mechi 19 wameisaidia kukusanya pointi 52 na mabao 48 ikiwa ndio timu yenye safu kali ya ushambuliaji lakini ikiruhusu mabao machache tisa.
Kwa upande wa Azam inayofuata kwa kufumania nyavu katika ligi ikiwa na mabao 45, licha ya kumkosa Dube aliyeifungia mabao saba, lakini bado ina majembe ya maana wakiongozwa na Fei Toto, Kipre Junior, Gjibril Sillah, Idd Seleman ‘Nado’, Abdul Suleiman ‘Sopu’ na Ayoub Lyanga ambao wameshirikiana kuifanya timu hiyo iwe tishio.
Safu za ulinzi za timu zote zitakuwa na kazi ya kuwachunga washambuliaji wa timu pinzani sambamba na kuwalinda makipa Diarra na Mustafa Mohammed ambao wamekuwa wakionyesha umahiri uwanjani kuzibeba timu hizo.
Timu zote zitawakosa baadhji ya nyota, Yanga ikikosa huduma ya kiungo mkabaji, Khalid Aucho na beki Kibwana Shomary aliyeumia juzi kwenyue mechi dhidi ya Geita Gold, wakati Azam haitakuwa na huduma ya Dube, Allasane Diao na nahodha Sospeter Bajana walio majeruhi wa muda mrefu.
Kwa aina ya soka la timu hizo ni wazi mashabiki wataendelea kupata burudani ya boli linalotembea na kuhesabu mabao kama ilivyokuwa kwenye mechi ya kwanza iliyopigwa Oktoba mwaka jana na Yanga kushinda mabao 3-2, huku Aziz KI akipiga hat trick.
ISHU YA DUBE NA FEI
Mechi ya kesho inazikutanisha timu hizo huku ukiwa na sakata la Prince Dube aliyeweka mgomo baridi akishinikiza kuondoka Chamazi, ikiwa ni miezi kadhaa tangu Feisal Salum ‘Fei Toto’ kufanya kitu kama hicho alipokuwa Yanga kabla ya kutua Azam baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuutaka uongozi wa Yanga kumalizana na nyota huyo.
Dube aliyerudisha kila kitu cha Azam na kuhamia hotelini baada ya kuaga rasmi kuonyesha yeye na Azam ndo imeisha, anahusishwa na Yanga, klabu inayoelezwa anaipenda tangu akiwa Zimbabwe na ndio maana mara kadhaa amekuwa akionekana uwanjani kuiangalia ikicheza.
Kitendo cha Fei Toto kuivuruga Yanga na kuibukia Azam kumemfanya nyota huyo kuonekana kuchukiwa na mashabiki wa timu hiyo ya zamani waliokuwa wakimzomea uwanjani na kesho atakuwa na kazi mbele ya mashabiki hao kwenye mechi hiyo huku jina la Dube huenda nalo likatawala Kwa Mkapa, hasa baada ya kuibuka taarifa kutoka kwa uongozi wa Azam kwamba klabu za Simba na Al Hilal ya Sudan zimepeleka ofa kumtaka nyota huyo Mzimbabwe.
MFUNGAJI BORA
Mechi ya leo mbali na vita ya pointi tatu kwa kila timu, lakini kuna ngarambe nyingine itakayowahusisha Fei Toto, Kipre Junior kwa upande wa Azam dhidi ya Stephane Aziz KI, Mudathir Yahya na Maxi Nzengeli katika ufungaji bora. Aziz KI ndiye kinara wa mabao kwa sasa wa Ligi Kuu akifunga 13, moja zaidi na aliyonayo Fei Toto wakiwa ni kati ya wachezaji vinawa waliohusika na mabao mengi kwa timu hizo.
Aziz KI licha ya kufunga mabao 13, ameasisti pia mara sita na kumfanya ahusike na mabao 19 akimpiku Fei Toto mwenye asisti tano na mabao 12 na kumfanya ahusike na mabao 17m wakati Kipre mwenye mabao sita na kuasisti nane ikiwa na maana amehusika mabao 14.
Pia Aziz, Fei na Kipre kila mmoja amefunga hat trick katika mechi za Ligi Kuu msimu huu sambamba na Waziri Junior wa KMC na Jean Baleke aliyekuwa Simba ambaye kwa sasa anakipiga katika Ligi Kuu ya Libya.
Hivyo mechi hiyo kila mchezaji atakuwa na kiu ya kuongeza idadi ya namba alizonazo katika mabao na asisti, sambamba na kuzibeba timu hizo zinazofundishwa na makocha wa kigeni, wenyeji Azam ikiwa chini ya Youssouf Dabo kutoka Senegal na Yanga ikiwa na Miguel Gamondi raia wa Argentina. Kipre ndiye mchezaji anayeongoza kwa asisti hadi sasa akifuatiwa na beki wa Yanga Yao Kouassi kuonyesha mechi ya kesho itakuwa burudani tamu kwa mashabiki watakaoenda uwanjani na wale watakaoifuatilia kupitia runinga.
NAMBA ZAIBEBA YANGA
Kwa kurejea kwenye rekodi baina ya timu hizo katika Ligi Kuu, namba zipo upande wa Yanga ambao imepata ushindi kwenye mechi 13, huku wapinzani wao wakishinda mara tisa, huku mechi nyingine tisa zikiishia kwa sare tofauti.
Pia Yanga imefunga jumla ya mabao 41 dhidi ya 37 ya Azam, lakini kwenye mechi sita za mwisho baina yao katika ligi, mabingwa wa kihistoria - Yanga, imeshinda nne na kufungwa moja, huku mchezo mmoja Azam ikitamba.
Rekodi zinaonyesha hakuna pambano baina ya Azam na Yanga katika Ligi Kuu limewahi kuvuka mabao matatu, licha ya kwamba kwa msimu huu timu hizo kila moja imewahi kupata ushindi wa mabao 5-0 mbele ya wapinzani wao, Yanga ikitoa dozi hiyo katika mechi nane tofauti za michuano yote, wakati Azam ikiinyoosha Mtibwa Sugar.
Yanga imezifunga timu za Asas ya Djibouti katika mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika, ikazinyoosha KMC, JKT Tanzania, Simba na Ihefu katika mechi za Ligi Kuu, pia ikaikamua Jamhuri kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 kisha kuzizabua Polisi Tanzania na Hausung zilipokutana kwenye mechi za Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
Hii ikiwa na maana moja ya timu hizo itakapofanya uzembe wa aina yoyote huenda historia ikaandikwa kwa mmoja kupigwa mabao mengi, ingawa sio kitu kinachotrajiwa sana kwa aina ya wachezaji wa timu hizo na pia mfumo wa makocha na ushindani uliopo baina ya timu hizo.
Vikosi vinavyoweza kuanza;
AZAM: Mohamed Mustafa, Lusajo Mwaikenda au Nathaniel Chilambo, Pascal Msindo, Yannick Bangala, Yeison Fuentes, James Akaminko, Yahya Zayd, Ayoub Lyanga, Gjibril Sillah, Feisal Salum na Kipre Junior.
YANGA: Djigui Diarra, Yao Kouassi, Joyce Lomalisa au Nickson Kibabage, Ibrahim Bacca, Dickson Job, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Kennedy Musonda, Stephane Aziz KI na Pacome Zouzoua.