BAADA ya kupoteza pointi tatu mbele ya Azam FC, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amemtupia lawama kwa waaamuzi wa mchezo huo akidai wameruhusu bao la pili ambalo inaonyesha kuwa mfungaji alikuwa ameotea.
Bao hilo lilifungwa na kiungo mshambuliaji Feisal Salum ‘Fei Toto’, dakika ya 51, Yanga ilipoteza pointi tatu mbele ya Azam FC kwa kukubali kichapo cha mabao 2_1, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.
Gamondi amesema mechi ilikuwa ya ushindani mkubwa na kipindi cha kwanza walicheza vizuri na kushindwa kutumia nafasi zilizopatikana.
Amesema wamefanya makosa katika boksi lao la Azam FC kufanikiwa kusawazisha na kipindi cha pili kutumia nafasi waliyoitengeneza na kupata bao la pili ambalo haikuwa sahihi.
“Bao la pili halikuwa sahihi, mfungaji aliotea ‘ Off Side’, waamuzi hili hawajaliona lakini ndio mpira, pia tumeongeza wachezaji majeruhi baada ya kulazimika kumtoa Pacome (Zouzoua) na Yao Attohoula ambao waliumia.
Wachezaji hao wako chini ya uangalizi na bado hatujapata taarifa juu ya jeraha lao, tumepoteza mechi na tunarejea katika uwanja wetu wa mazoezi kuangalia tulipokosea,” amesema kocha huyo.
Kuhusu hali ya kiungo wao, Khalid Aucho, Gamondi amesema nyota huyo unaendelea vizuri na matarajio yake kuonekana katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Amesema Aucho anaendelea vizuri na ameshaanza mazoezi mapesi kwa akiwa Gym chini ya uangalizi na baada ya muda mfupi atarejea uwanjani kufanya mazoezi ya ushindani na mechi ya Kimataifa atakuwa sehemu ya kikosi.
“Natarajia Aucho atakuwa sehemu ya kikosi katkka mchezo wetu ujao, kwa sababu tayari ameshaanza mazoezi mepesi, lakini pia tunasubiri taarifa kutoka kwa daktari juu ya asilimia ya kupona na kuweza kucheza mechi hiyo ya ushindani,” amesema Gamondi.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns, amesema anawapa mapumziko mafupi wachezaji kwa sababu tangu walipomaliza mechi ya ya makundi dhidi ya Al Ahly hawajapata muda wa kupumzika.
Gamondi ameeleza kuwa baada ya mapumziko mafupi watarejea uwanja kujiandaa na mchezo wa Mamelodi Sundowns ambao ni timu yake ya zamani ambayo aliwahi kuifundisha.
Ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema taarifa juu ya ukubwa majaraha na muda gani watakuwa nje ya uwanja kwa Pacome aliyeumia goti na Attohoula Enka itajulikana kesho baada ya kupata vipimo.
“Ni kweli Pacome na Attohoula walishindwa kumaliza mchezo kwa sababu ya kuumia ambapo mmoja aliumia goti na mwingine Enka, kwa taarifa za daktari hadi saa 72 baada ya mchezo wetu dhidi ya Azam FC,” amesema Kamwe.