EWURA imesema Mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi March 2024 yamechangiwa na ongezeko la bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FOB) kwa wastani wa asilimia 4.5 kwa mafuta ya petroli na asilimia 1.99 kwa mafuta ya dizeli na kupanda kwa gharama za uagizaji wa mafuta (premiums) kwa Bandari ya Dar es Salaam kwa wastani wa 15.38 kwa petroli na asilimia 40.41 kwa dizeli na kwa Bandari ya Mtwara kwa wastani wa asilimia 7.61 kwa petroli na dizeli.
EWURA imesema mabadiliko ya bei za mafuta yamechangiwa pia na ongezeko la matumizi ya EURO katika kulipia mafuta yaliyoagizwa.
Itakumbukwa bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini kwa mwezi uliopita zilizoanza kutumika kuanzia Jumatano February 07, 2024 saa 6:01, bei za rejareja za mafuta katika Mkoa wa Dar es salaam petrol ilikuwa ni Tsh. 3051 kwa lita, dizeli Tsh. 3029 na mafuta ya taa 2840.