Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha ameondoka leo Jumatano, Februari 7, 2024 kwenda nchini kwao Algeria kushiriki kozi kozi ya ukocha ya siku tano hivyo hatakuwa sehemu ya benchi la ufundi la timu hiyo katika mechi mbili za Ligi.
hayo yamesemwa leo na Meneja wa habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally wakati akizungumza na Simba Media kufuatia safari hiyo ya kocha wao mkuu.
Benchikha anaondoka nchini ikiwa ni saa chache baada ya timu yake ya Simba kupoteza mchezo wa Ligi dhidi ya Tanzania Prisons kwa kukubali kichapo cha bao 2-1 jana katika Dimba la CCM Jamhuri Morogoro.
“Mwalimu Benchikha ameondoka leo kwenda nyumbani kwao Algeria ambako anaenda kushiriki kozi ya siku tano akiwa nchini humo. Maana yake ni kwamba atakosa michezo miwili ya Ligi Kuu, mchezo dhidi ya Coastal Union (Machi 9) na mchezo dhidi ya Singida FG FC (Machi 12).
“Katika kipindi chote hicho ambacho mwalimu Benchikha hatakuwa nchini Tanzania, atakuwa nje na majukumu yake ndani ya Simba, mikoba na majukumu yake amemwachia msaidizi wake namba moja, Kocha Farid ambaye ni kocha mwenye uzoefu wa muda mrefu.
“Farid amekuwa msaidizi wa Benchikha na msaada mkubwa kwake kwa muda mrefu. Mwalimu Farid ataendelea kusaidiana na mwalimu Selemani Matola ambaye wamekuwa wote tangu alipokuja hapa Tanzania.
“Mchezo wa Machi 15, dhidi ya Mashujaa FC kocha Benchikha atakuwa kwenye benchi la ufundi kuendelea na majukumu yake,” amesema Ahmed Ally.