Daktari wa Young Africans SC, Moses Etutu, amezungumzia hali ya majeruhi ya wachezaji wa kikosi hicho ambao ni Kibwana Shomari, Khalid Aucho na Zawadi Mauya.
Kwa muda mrefu, Mauya amekosekana uwanjani kutokana na kusumbuliwa na majeraha, huku Aucho akifanyiwa upasuaji wa goti hivi karibuni, wakati Kibwana akiumia enka katika mchezo wa jana dhidi ya Geita Gold.
Akizungumzia hali za wachezaji hao, Daktari Etutu ameanza kuzungumzia hali ya Kibwana akisema:
“Kwa sasa tumeweza kumfanyia baadhi ya vipimo kuweza kujiridhisha kuona hasa ni shida gani ilikuwa ikimsumbua kwa sababu alipata majeraha wakati akicheza na kuumia kifundo cha mguu wake wa kulia.
“Tumefanya baadhi ya vipimo na tumejiridhisha amepata ‘ankle tosun’ or ‘ankle sprain’ (jeraha ambalo hutokea pindi kifundo cha mguu kinapozunguka au kugeuka kwa njia isiyo ya kawaida) ambayo inaweza kumuweka nje kwa muda wa wiki mbili hadi tatu, lakini kwa matibabu mazuri tuliyonayo tunaamini atarejea kabla ya huo muda na ataendelea kuitumikia timu yake bila ya shida yoyote.”
KHALID AUCHO
Kwa upande wa hali ya Aucho, Daktari Etutu, amesema: “Kwa sasa ‘recovery session’ yake ipo vizuri sana, ana imarika sana kuliko tulivyotarajia, hii inatokana na matibabu anayoyapata.
“Alifanyiwa upasuaji wa goti, akaanza na program ya kunyoosha viungo ambayo tuliigawa wiki ya kwanza alikuwa akiifanya kwa ajili ya kusaidia kupata uwezo wa kutembea, kuanzia Jumatatu tunatarajia anaweza kuja huku uwanjani kufanya mazoezi mepesi ya uwanjani ili kusaidia kuimarika.
“Wiki inayofuata itakuwa sasa anafanya mazoezi ya fitnes (utimamu wa mwili) na mazoezi kama ya wachezaji wengine wanavyofanya, kwa hiyo ana imarika kwa uharaka sana kuliko tulivyotarajia lakini tunaendelea kumuombea Mungu ili aweze kusaidia kurejea mapema zaidi ya muda pengine na huo tuliotegemea angeweza kurejea.”
GIFT MAUYA Ishu ya Mauya, nayo Daktari Etutu anafafanua hivi: “Kwa sasa tunaweza kusema Mauya ameshatoka kwenye chumba cha matibabu kwa sababu majeraha aliyoyapata yameshapona na sasa yupo na kocha wa utimamu wa mwili kwa sababu alikuwa nje ya mazoezi muda fulani, hivyo huwezi kurejea ghafla kwani unaweza kusababisha majeraha zaidi.
“Hivyo lazima aanzie kwa kocha wa utimamu wa mwili ili kumsaidia kupata utayari wa mwili kwa ajili ya mechi au mazoezi mengine magumu. Kwa hiyo sasa hivi yupo sawa kabisa na anaendelea na kocha wa utimamu wa mwili.
“Tofauti na wachezaji hao watatu, hatuna mchezaji mwenye majeraha makubwa zaidi, kuna magonjwa tu ya kawaida kama red eyes ambayo ndani ya siku mbili yashapona, hivyo hakuna majeraha yanayoweza kuwafanya washindwe kucheza mechi au kutimiza majukumu yao, wana matatizo madogomadogo tu ambayo tunayatibu na yanaisha bila shida yoyote.”