Edo Kumwembe Ainunua Kesi ya Prince Dube "Ni mwendo wa Kisasi tu"

 

Edo Kumwembe Ainunua Kesi ya Prince Dube "Ni mwendo wa Kisasi tu"

Lilikuwa suala la muda tu kabla mlango haujafunguliwa tena. Ilianzia kwa ‘mjukuu wa Sultan’ Fei Toto. Aliufungua mlango wa kujiondokea klabuni muda wowote aliojisikia. Na sasa ‘Mtoto wa Mfalme’, Prince Dube amefuata nyayo. Lilikuwa suala la muda tu.


Mwishoni mwa Desemba mwaka jana, Yanga wakiwa katika michuano mitatu tofauti, Feisal aliamua kuchukua Shilingi 112 milioni kutoka kusikojulikana akaziweka katika akaunti ya Yanga. Akaacha na barua yenye kusudio la kuvunja mkataba kwa madai ya kunyanyaswa klabuni. Kwamba hakuwa na furaha.


Bahati mbaya mlango wake haukufungwa vema. Kulikuwa na kesi ambayo iliishia njiani. Tatizo la muda liliamuliwa na Mama yetu Samia Suluhu pale Ikulu alipotaka Yanga watatue tatizo lake. Kauli ya Rais ni amri. Kesho yake tu Yanga walionekana mezani na Feisal na kumruhusu kwenda alikotaka. Alikotaka? Hapana. Kwenda Azam.


Ninachoamini, kama ile kesi ingetolewa hukumu kwa wazungu basi Fei angeendelea kuwa mchezaji wa Yanga hadi leo. Wazungu wangeangalia vitu vichache vya msingi. Wakati anasaini mkataba na Yanga aliwekewa bastola kichwani? Hapana! Alikuwa ananyimwa mishahara? Hapana! Alikuwa hapangwi? Hapana! Kesi isingefika mbali.


Labda kwa kesi kutofika katika mikono ya uamuzi wa wazungu ndio maana Prince naye kafuata njia hii. Mwanzoni mwa Machi ameamua kuandika barua ya kutaka mkataba wake na Azam usitishwe. Kisa? Hana furaha klabuni hapo. Nasikia amewasumbua kwa muda mrefu.


Bahati nzuri Azam wametumia busara kubwa kumkubalia moja kwa moja. Lakini subiri kwanza. Maswali yanabakia yale yale ambayo tulijiuliza kwa Fei. Dube halipwi mshahara wake? Analipwa. Hapangwi? Anapangwa. Hata kama ana msuguano na kocha wake, lakini anapangwa. Vinginevyo Azam wangeweza kuweka ngumu na Dube asingekuwa na lolote la kufanya. Wangeweza kuweka ngumu walau hadi mwisho wa msimu.


Azam bado wanapambana na Simba na Yanga katika kilele cha Ligi Kuu na watachuana nao katika michuano ya Shirikisho (ASFC) mbele ya safari. Hata hivyo, wamemwambia Dube apeleke pesa zao aondoke zake salama bin salimini. Ni sawa kwao, lakini haina afya katika mchezo wa soka hapa nchini. Taratibu lazima zifuatwe.


Mchezaji anapoamua kuondoka zake wakati michuano mbalimbali ikiendelea huku yeye akiwa mchezaji muhimu sio haki. Na itaendelea kutokea sana kwa sababu tuliifurahia kesi ya Fei kinazi, lakini hapo hapo hatukufika mwisho mzuri kwa sababu Yanga walilazimika kinyonge kumruhusu Fei baada ya Mama kutoa neno lake Ikulu.


Mchezaji anapoamua kuondoka katikati ya msimu huku kukiwa hakuna dirisha lililo wazi nini maana yake? Klabu haina muda wa kuziba pengo lako. Jaribu kumfikiria Fei, jina lake lilishakwenda CAF kama mchezaji wa Yanga. Lakini lilikuwepo pia katika michuano mbalimbali. Yanga wangepata wapi mrithi wake kwa wakati huo? Hapo ndipo Wazungu wangeiamua kesi yake kwa urahisi. Labda kama angekuwa hachezi.


Neno ‘ukosefu wa furaha’ linatumika vibaya. Inafika mahali ambapo mchezaji hana uhusiano mzuri na kocha anadai hana furaha. Vipi kama hana uhusiano mzuri na kocha, lakini ana uhusiano mzuri na viongozi pamoja na wachezaji wenzake? Vipi kama ni kinyume chake? Kwamba ana uhusiano mzuri na kocha lakini hana uhusiano mzuri na uongozi ingawa analipwa mshahara wake?


Sio wachezaji wote wana furaha klabuni, lakini huwa hawahami kihuni. Pale Arsenal, ghafla kocha wa Arsenal, Mikel Arteta anampiga benchi kipa wake bora wa msimu uliopita, Aaron Ramsidale. Anampanga David Raya. Unadhani Ramsidale ana furaha na Arteta? Lakini hakuna namna. Hawezi kutaka kuvunja mkataba wake ghafla ghafla. Nadhani atasubiri hadi mwishoni mwa msimu. Ndivyo wanavyofanya wenzetu.


Lakini kwa sisi nadhani wengi tungemsapoti Aishi Manula kuvunja mkataba katikati ya msimu kwa sababu tu kocha Benchikha ameamua kumpanga Ayoub Lakred na kumfanya Aishi kuwa kipa wa pili. Kama Aishi atataka kuondoka haiwezi kuwa sasa. Anapaswa kusubiri hadi mwishoni mwa msimu mwa msimu.


Dube ameamua kuanzisha vurugu hizi kwa sababu anajua kwamba kwa Tanzania kila kitu kinawezekana. Inawezekana kuna watu wapo nyuma yake. Mbona hata kwa Fei minong’ono ilionyesha kwamba kuna watu wapo nyuma yake na baadaye ikadhihirika kwamba ni kweli kulikuwa na watu nyuma yake. Tatizo tunaendesha mpira wetu kihuni na sisi wenyewe tumekubali iwe hivi.


Wachezaji wanavimba kichwa na kuua kabisa uhusiano wao na mabosi wao wakiamini kwamba moja kwa moja wanahamishia riziki zao kwingineko. Fei alidai kwamba mabosi wa Yanga walikuwa wanamlisha ugali na sukari, akadai kwamba wanampuuza hawapokei simu zake.


Leo Dube anadai kwamba kuna viongozi wa Azam ni mashabiki wakubwa wa Simba na Yanga na wanafurahi hizo timu zikishinda. Kwanini aseme yote haya? Anajaribu kwa nguvu zote kuvunja daraja la uhusiano baina yake na mabosi wa Azam. Sidhani hata kama watakuwa na uhusiano wa kawaida baina yao.


Kitu kingine kinachonishangaza kuhusu wachezaji hawa ni ukweli kwamba hawajui kuwa wanarudisha nyuma vipaji vyao pindi wanapogoma. Kwanini wasimalize msimu ili hata wanakoenda wawe fiti bila ya kuandaliwa programu maalumu. Fei alinenepa alipoikacha Yanga na kuanza kuzurura Forodhani.


Makocha wa Taifa Stars walilazimika kumpangia programu maalumu kule Ismailia Misri wakati wa maandalizi ya pambano la kufuzu Afcon dhidi ya Uganda, lakini haikusaidia. Alionekana mzito. Angeweza kuweka siri yake moyoni hadi mwishoni mwa msimu na kisha kufanya vurugu ambazo alifanya. Ingeweza kuwasaidia hata Azam wenyewe.


Endapo Azam wakiuchana mkataba wa Dube, leo inamaanisha kwamba Dube atakuwa hana timu hadi Juni. Miezi mitatu. Anaweza kusaini mahali leo na akatangazwa lakini ataishia kufanya mazoezi tu. Itamuondolea ufiti wake. Mazoezi sio sawa sawa na mechi kwa sababu hata Fei alikuwa anafanya mazoezi Zanzibar. Ni kama ilivyowahi kumkuta Ramadhan Kessy aliyezingua Simba akitaka kwenda Yanga. Akasaini mkataba, lakini kilichotokea alifungiwa kucheza na kulimwa faini hadi hukumu ilipoisha ndipo alirejea uwanjani. Hii inasaidia nini kama inavuruga kipaji cha mhusika?


Tusipokuwa makini na jambo hili nadhani litaendelea kwa muda mrefu ujao. Haya ni mambo ya kizamani na hata hapo zamani wachezaji walitumia busara kusubiri nyakati zikifika. Mfano ni marehemu Method Mogella. Alicheza Simba akiwa mnazi wa Yanga. Walipojaribu kumfuata acheze kinazi akiwa na jezi ya Simba alikataa. Aliwaambia Yanga wasubiri muda wao ukifika atajiunga nao.


Kwanini wachezaji wa kisasa wanashindwa kusubiri? Rafiki yangu Bernard Morrison yeye alikuwa anakwenda mbali zaidi kwa kuanzisha vituko vingi kambini ili mradi tu mabosi wake wajue kwamba ana mpango wa kuondoka zake. Fikiria kwamba yeye na Dube ni wachezaji wa kigeni. Wanawafundisha nini wachezaji wengine?


Tumsubiri mchezaji mwingine wa tatu ambaye atafuata baada ya Fei na Dube. Kinachoonekana hata mabosi wa klabu hizi wameanza kufurahia sinema hizi. Na kuanzia sasa zitakuwa zinakwenda kwa mwendo wa kisasi tu. Kama uliwahi kunifanyia hivi basi mimi nitakufanyia vile.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad