Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema huwa anakataa kupokea mahari kwa ajili ya binti zake, badala yake hulipa mahari kwa familia za vijana wa kiume wanaooa kwake.
Hii ni kinyume na mila na desturi za Kabila la Wanyankole anakotokea Museveni, familia ya bwana harusi mtarajiwa ndio hulazimika kulipa mahari kwa familia ya bibi harusi.
Museveni ambaye ameshaozesha mabinti watatu na kulipa mahari, amesema lengo la hatua yake hiyo ni kutoa somo la mabadiliko kwa jami kutambua kwamba kama inataka kupambana na unyanyasaji wa kijinsia na kufikia uwezeshaji wa wanawake, ni vyema msichana aende 'kibabe' kwa mumewe.
Museveni alibanisha hayo jana Machi 8, 2024 wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, akisema familia nyingi za Wanyankole ambazo zimetajirika kutokana na ufugaji wa ng'ombe kibiashara chini ya uongozi wake, zimeachana na tabia ya kutoa na kuomba mahari, hususani ng'ombe.