Gamondi Afafanua Sababu ya Kuwarudisha Bacca, Mudathir

Gamondi Afafanua Sababu ya Kuwarudisha Bacca, Mudathir


Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amewaita fasta mastaa watatu wa kikosi chake cha kwanza kati ya watano wazawa waliokuwa wameitwa kwenye timu ya taifa 'Taifa Stars' huku Djigui Diarra, Pacome Zouzoua wakikwama.


Stars ipo Azerbaijan kwaajili ya mechi za FIFA Series ambazo ni mashindano madogo mbadala wa mechi za kirafiki za kimataifa na imecheza mechi mbili ambapo ya kwanza ilifungwa bao 1-0 na Bulgaria na ya pili leo imeikanda Mongolia mabao 3-0.


Yanga ikiwa imebakiza siku nne kuikabili Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika mchezo wa robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, Gamondi amewaita mastaa wake watatu tayari kwa kuandaa jeshi la kumaliza mchezo huo mapema Jumamosi ya wiki hii.


Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi amesema amemrudisha Mudathir Yahya, Clement Mzize na Ibrahim Abdallah 'Bacca' haraka kwasababu ana mpango nao katika mechi ijayo.


Alisema kwa mujibu wa TFF walimtaka kuwarudisha wachezaji ambao ni muhimu kikosini hivyo na yeye akafanya hivyo huku akimuacha nahodha Bakari Mwamnyeto na kipa Abuutwalib Mshery.


"Ujio wa Bacca, Mudathir na Mzize umeongeza chachu ya maandalizi mazuri kwani umeongeza idadi ya wachezaji katika kila eneo, ukuta sasa umekamilika, kuna Dickson Job ambaye amekuwa akicheza sambamba na Bacca," alisema na kuongeza;


"Eneo la ushambuliaji ambalo lilikuwa linamkosa Mzize na Kennedy Musonda sasa mmoja karudi kuziba nafasi huku kiungo ameongezeka Mudathir ambaye nimekuwa nikimtumia mara kwa mara kikosini," alisema.


Alipoulizwa juu ya mastaa wake wa kigeni ambao pia wapo timu za taifa, Djigui Diarra, Musonda, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki alisema hao watarudi mara baada ya kumaliza mechi zote mbili.


"Sina wasiwasi na ubora wa wachezaji hao wana uzoefu mkubwa na wanajua nini wanakifanya wakipewa majukumu uwanjani, naamini hata wasipofanya mazoezi muda mrefu watafanya kazi nzuri," alisema na kuongeza;


"Hakuna asiye tambua ubora wa Diarra awapo langoni lakini pia viungo wawili Pacome na Aziz Ki ni wachezaji wazuri na wazoefu, naamini kutokana na kutambua mfumo wa timu na huko walipo kupata nafasi ya kucheza, watarudi na kufanya vizuri kwenye mchezo ujao."


Mwanaspoti lilimtafuta Bacca ambaye alikiri kuwa tayari wamerejea nchini na wameanza mazoezi tayari kwa mchezo huo utakaopigwa Jumamosi.


"Nipo Tanzania tangu jana, ila sijaanza mazoezi, nitaanza leo lakini wenzangu tayari wameshaanza mazoezi, kutokuanza kuna sababu binafsi siwezi kuweka wazi," alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad