Hali ya upatikanaji huduma kwa wagonjwa wenye kadi za NHIF

Hali ya upatikanaji huduma kwa wagonjwa wenye kadi za NHIF


Wakati baadhi ya hospitali binafsi zikisitisha huduma kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), wananchi wameeleza namna walivyoathiriwa na uamuzi huo, wengine wakilazimika kutumia fedha taslimu kupata matibabu.


Hospitali ambazo zimesitisha huduma leo, Machi mosi, 2024 ni utekelezaji wa tamko lililotolewa na Vyama vya Watoa Huduma Binafsi za Afya nchini (APHFTA) kupinga kitika kipya cha mafao kilichotolewa na NHIF ambacho matumizi yake yameanza leo.


Februari 29, 2024, Mwenyekiti wa APHFTA, Dk Egina Makwabe alieleza msimamo wao wa kutokubaliana na mabadiliko yaliyofanywa kwenye kitita hicho.


Kupitia mitandao ya kijamii, hospitali za Kairuki, Regency na TMJ zimeeleza wazi kusitisha kutoa huduma kwa wagonjwa wenye kadi za NHIF.


Hata hivyo, NHIF imetoa taarifa kwa umma ikiwataka wanachama wake kutumia vituo mbadala wa vile vilivyotangaza kusitisha huduma.


Cardinal Rugambwa Hospitali ya Cardinal Rugambwa, iliyoko Ukonga, Dar es Salaam inaendelea kutoa huduma kwa wanachama hao.


Zabron Mushi, mkazi wa Mongo la Ndege amesema amelazimika kupiga simu kabla ya kwenda hospitalini hapo leo.


"Huwa nahudhuria kliniki hapa ya ugonjwa wa presha kila Ijumaa, hivyo kutokana na tangazo lile niliona nipige simu kuuliza kabla sijachoma nauli yangu na kupoteza muda, waliponijibu huduma ipo ndiyo nikaja,” amesema Mushi.


Rehema Fadhili, mkazi wa Gongo la Mboto, amesema alikuwa na mgonjwa nyumbani anayetakiwa kwenda hospitali binafsi iliyopo katikati ya jiji, lakini baada ya kuona tangazo ameshindwa kumpeleka.


Badala yake Rehema amesema imebidi aende hospitalini hapo kuuliza kama kuna huduma kwa kuwa mgonjwa wake ni wa kubebwa.


"Nimefika hapa nikauliza nikaambiwa wanapokea kadi za NHIF, hivyo nimewapigia simu nyumbani wamuandae mgonjwa niende nikamchukue aje kupata matibabu," amesema Rehema.


Katibu wa hospitali hiyo, Honest Antony, amesema wanaendelea na huduma kutokana na msimamo wa umoja wa hospitali zinazosimamiwa na taasisi za dini za Kikristo unaowataka kuendelea kutoa huduma mpaka pale itakapoamuliwa vinginevyo.


Antony amesema wamepata tangazo la msimamo huo jana, Februari 29, 2024 kupitia Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya huduma za Kijamii (CSSC), Dk Peter Madaki.


Hali ilivyo Aga Khan Akizungumza na Mwananchi Digital katika Hospitali ya Aga Khan, Catherine Masawe amesema ameshtuka baada ya kufika hapo na kuambiwa hakuna huduma kwa wenye kadi za NHIF.


"Nimefika hapa mapema sikuwa na taarifa, lakini hii imeniathiri kwa kuwa nawaza kwenda hospitali nyingine na matibabu yangu yamebakiza siku chache," amesema Catherine na kuongeza;


"Ni bora tungeambiwa muda mrefu ili tujipange, sasa tumeshtukizwa maana wengine huduma tumezianzia hapahapa na inapaswa kuendelea nazo hapa hadi pale tutakapomaliza," amesema.


Ameiomba Serikali itatue suala hilo kwa kuwa hospitali binafsi zinawasaidia kutibiwa kwa haraka.


Hata hivyo, amesema endapo suala hilo halitapatiwa ufumbuzi hatakuwa na namna zaidi ya kwenda hospitali nyingine.


"Wangetupa muda hata wa mwezi mmoja tujipange, lakini hii tumeona jana kwenye habari na leo wamesitisha, tunawaza gharama ni kubwa," amesema.


Kwa upande wao, ndugu wawili, Glory na Samira Mwamba, wamesema wamelazimika kutumia fedha taslimu kupata huduma ya matibabu ya mama yao aliyekuwa akipata huduma kupitia NHIF.


"Serikali iingilie kati suala, hili tutapoteza ndugu zetu kwa kweli," amesema Glory.


"Sisi tunaenda nyumbani tu maana hapa tumekuja wamesema menejimenti ya hospitali inakaa kikao hadi itakapokuja na majibu, nilikuja kuhudhuria kliniki," anasema mgonjwa ambaye hakutaka jina liandikwe gazetini.


Marie Stopes Hospitali ya Marie Stopes ya Sinza imeendelea kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF, uongozi ukisema utatoa tamko baadaye.


Mkuu wa mawasiliano wa taasisi ya Marie Stopes, Oscar Kimaro amesema: "Tunaendelea kuwasiliana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Aphfta na Wizara ya Afya kisha tutatoa tamko baadaye (leo au kesho)."


Kimaro amesema licha ya wao kuendelea na huduma, lakini kitita kipya kilichoboreshwa cha NHIF hakina masilahi kwao, hivyo wanahitaji kukaa na wahusika kujadili suala hilo.


"Ni fursa ya kukaa na wahusika kujadiliana kuhusu mustakabali wa jambo hili, tunachotaka ni kuwasilisha hoja zetu, ili tupate muafaka na wananchi wapate kunufaika na huduma zetu, kwani hospitali binafsi zimekuwa na mchango mkubwa kwenye sekta ya afya," amesema Kimaro.


Mwanachama wa NHIF ambaye hakutaka jina lake kuwekwa wazi, aliyefika katika hospital hiyo amesema ametumia kadi yake kupata matibabu. "Nimeanza kupata matibabu kupitia bima yangu na nimepokewa vizuri tu," amesema.


Wagonjwa wanaotumia bima ya NHIF wakiwa wanajiandikisha katika Hospitali ya Hindu Mandal leo Ijumaa Machi mosi, 2024. Picha Devotha Kihwelo.


Hindu Mandal Hospitali ya Hindu Mandal kwa upande wake imeendelea kutoa huduma kwa wanachama wanaotumia bima ya NHIF.


Lucy Kalinga, mkazi wa Kigamboni amesema aliposikia taarifa za kusitishwa kwa huduma kwa wenye kadi za NHIF alijikuta akikata tamaa ya kutibiwa.


"Nilimuomba Mungu anisaidie wakati nakuja hospitali hii wasiwe wamesitisha huduma, maana nimeona hospitali nyingine za binafsi wamefanya hivyo, lakini nimefika hapa nimepokewa na kwenda kumuona daktari," amesema Lucy. Hospitalini hapo hakuna mabango ya kusitishwa kwa huduma.


Hospitali ya Regency Regency imesitisha huduma kwa wenye kadi za NHIF, hali iliyosababisha baadhi ya wananchi waliofika kupata huduma kupiga simu kwa ndugu na jamaa wakiwaeleza wanatakiwa kulipia fedha taslimu.


Kwa kawaida hospitalini hapo ifikapo saa moja asubuhi kunakuwa na watu wengi kwenye foleni wakisubiri huduma, lakini leo hali ni tofauti.


Licha ya hospitali hiyo kutoa tangazo tangu jana Februari 29, 2024 kwamba haitawapokea wanachama wa bima wa NHIF, wapo baadhi waliofika hapo. Waliofika hospitalini hapo waliishia kwa mlinzi.


Unatumia bima? swali la kwanza la mlinzi wa hospitali ya Regency pindi mgonjwa anapoingia getini na endapo jibu litakuwa ndiyo, kwa maelezo mafupi anasema hakuna huduma hiyo kwa sasa.


Watoa huduma za NHIF waliokuwepo hospitalini hapo waliwapatia maelekezo ama wanaweza kugharamia huduma au kwenda katika hospitali nyingine zinazotoa huduma kwa wanachama hao, zikiwamo za Serikali.


Asha Mohamed, mkazi wa Kariakoo amesema amefika hospitalini hapo kwa kuwa hakuna na taarifa za kusitishwa huduma, kwani si mfuatiliaji wa taarifa za habari wala kutembelea mitandao ya kijamii.


"Nimefika hapa nashangaa mlinzi ananiuliza kama natumia bima nimemwambia ndiyo kaniambia hakuna huduma kwa sasa nimebaki nashangaa," amesema Asha. Amesema amebaki njiapanda, kwani amekuwa na utaratibu wa kuonana na daktari kila baada ya wiki mbili kutokana na tatizo alilonalo.


"Nimechanganyikiwa kitu ambacho sielewi ni ufumbuzi wa tatizo langu hapa, nilishapima vipimo vitatu na kwa maelezo ya mlinzi kaniambia naweza kutumia hospitali za Serikali," amesema.


Hilda Samota, mkazi wa Magomeni amesema amefika hospitalini hapo kwa ajili ya kliniki, lakini ameambiwa huduma hakuna anatakiwa kulipia zote atakazopatiwa.


"Leo ni siku yangu ya kliniki nafika hapa naambiwa nilipie wakati nina bima, imebidi nimpigie simu mume wangu kumwambia, ameniambia niendelee na vipimo," amesema.


Kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo, Cecilia Swai amesema wameambiwa hadi kesho Machi 2, 2024 wajue njia mbadala ya kumtibu ndugu yao, kwani watasitisha huduma.


"Dada yangu amelazwa hapa, lakini tumepewa hadi kesho tuwe tumejua tunaendelea naye vipi kwenye malipo ya matibabu kwa kuwa bima yetu haitatumika tena hapa au tumuhamishe hospitali nyingine," amesema Cecilia.


Hospitali ya Rabininsiana Kitengule Katika hospitali za Rabininsia Memorial na Kitengule zilizopo Tegeta zinaendelea kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF.


Baadhi ya waliofika hospitalini hapo waliuliza kwa wahudumu iwapo wanachama wa NHIF wanapokewa.


Baada ya kupatiwa majibu walielekea dawati maalumu linalohusika na bima hiyo kwa ajili ya kufuata utaratibu.


"Nimekuja asubuhi nimepata huduma kama kawaida kupitia NHIF. Nilikuja kuangalia afya yangu nimepokewa vizuri na baada ya kufuata taratibu zote nilipewa huduma," amesema Joel Mallya.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad