Kilichotokea Saa za Mwisho za Rais Magufuli Kabla Hajafariki, Mabeyo Asimulia

 
"Siku moja kabla ya kifo chake hali ilibadilika kidogo na yeye alijitambua kwamba hali imebadilika, na nadhani alijua Mwenyezi Mungu alimuongoza kwamba hatapona alichosema nirudisheni nyumbani nikafie nyumbani... nikasema mheshimiwa hapana hapa upo kwenye mikono salama madaktari wapo waendelee kukutibu."

"Niseme jambo moja ambalo halikuwahi kusemwa huko nyuma kwa sababu nilikuwepo pale aliniita CDF (Mkuu wa Majeshi) njoo, akaniambia siwezi kupona, waamuru hawa madaktari wanirudishe nyumbani nikamwambia mheshimiwa sina mamlaka hayo, akasema yaani CDF unashindwa kuwaamuru madaktari wanirudishe nyumbani, nikamwambia suala la afya siyo la CDF mheshimiwa naomba ubaki utulie madaktari watatuambia."

"Alipoona kwamba nimekuwa na msimamo huo akaniambia niitieni paroko wangu, Paroko wa St. Peters Father Makubi lakini akaongeza akasema namuomba Kadinali Pengo naye aje hiyo ni asubuhi sasa tukamtafuta Pengo alikuwa kwenye ibada hakupokea, akaniuliza CDF haujampata Pengo? Nikamwambia yuko kwenye ibada baba atakapotoka atakuja, kwahiyo wakaja wote Kadinali Pengo na Father Makubi sasa katika taratibu za kikatoliki wanamsalia ibada na kumpa sakramenti ya upako wa magonjwa aliyekuwa katika hatari ya kufariki."
"Walipomaliza kumsalia akapumzika lakini ilipofika saa nane mchana wakatupigia watu wa hospitali wakanipigia mimi kama Mkuu wa Majeshi, wakampigia DGS na IGP wakatuambia hali ya mheshimiwa siyo nzuri sana hebu njooni, tukaenda tukamkuta ametulia lakini alikuwa hawezi kuongea tena, tukawaita madaktari wengine, nakumbuka tulimuita Profesa Maseru, Profesa Janabi alikuwepo muda wote kwa hiyo yule aliongezea nguvu wakajaribu kumuangalia, tukaendelea kukaa mpaka jioni, ikafika jioni saa kumi na mbili na nusu hivi au saa moja kasoro akakata roho, tukiwepo wakuu wa ulinzi wa vyombo watatu mimi (CDF), IGP na DGS" - Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo.

Jenerali Mabeyo ameyasema hayo katika mahojiano na Daily News Digital ikiwa ni kumbukumbu ya kifo cha Rais Dkt. John Magufuli aliyefariki dunia tarehe 17.3.2021

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad