KOCHA wa Azam Dabo na Gamondi wa Yanga Wapigana Mkwara Mechi ya Leo

 

KOCHA wa Azam Dabo na Gamondi wa Yanga Wapigana Mkwara Mechi ya Leo

Wakati kocha wa Yanga, Miguel Gamondi na mpinzani wake wa Azam FC, Youssouf Dabo wametembezeana mikwara wakijiandaa na mechi yao ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa leo usiku, rekodi zinaonekana sio rafiki sana kwa matajiri wa Lambalamba wakiivaa timu ya Wananchi uwanjani hapo.


Rekodi za Uwanja wa Mkapa zinaibeba zaidi Yanga mbele ya Azam kwani kwenye mechi nane za hivi karibuni timu hizo zilipokutana Yanga ameshinda mechi tano huku Azam FC ikishinda moja na sare mbili.


MECHI 8 ZILIZOPITA KWA MKAPA


Desemba 25, 2022: Yanga 3-2 Azam FC


Aprili 6, 2022: Azam FC 1-2 Yanga


Novemba 25, 2020: Yanga 1-0 Azam FC


Januari 18, 2020: Azam 1-0 Yanga


Aprili 29, 2019: Yanga 1-0 Azam FC Januari 27, 2018: Azam 1-2 Yanga


Oktoba 16, 2016: Yanga 0-0 Azam FC


Machi 5, 2016: Azam FC 2-2 Yanga


Mara ya mwisho Yanga kucheza kwenye uwanja huu dhidi ya Azam ilikuwa ni Oktoba 23 mwaka jana ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 na sasa wanaingia wakiwa wanaongoza ligi kwa pointi 52 wakiwaacha nyuma Azam FC kwa pointi nane huku Wananchi wakiwa nyuma kwa mchezo mmoja.


Azam FC ambao ndio wenyeji wa mchezo huu, wamecheza mechi 20 na kukusanya pointi 44 huku vinara wa msimamo Yanga wakicheza mechi 19 na kukusanya pointi 52.


Mchezo huo unasubiriwa kwa hamu kubwa na tayari umeanza kubeba taswira ya ubingwa, lakini Yanga wametamka kwamba kila mchezo kwao ni fainali na wanataka kutangaza ubingwa mapema, huku Azam FC wakitamba kuzitaka pointi tatu ili kurudisha matumaini ya ubingwa.


Kocha mkuu wa Azam FC, Youssouf Dabo alisema wao kama benchi la ufundi wamefanya kazi yao kwa usahihi kilichobaki ni wachezaji kufanya kazi yao huku wakitakiwa kutorudia makosa waliyoyafanya katika mchezo uliopita.


"Tunahitaji pointi tatu, sio rahisi lakini tumejiandaa kuhakikisha tunakuwa imara, lengo ni kupata ushindi ili kujirudisha kwenye ushindani wa kupagania taji," alisema na kuongeza;


"Yanga ni timu nzuri ina wachezaji wazuri, tutaingia kwa kuwaheshimu na sisi tukiwa tumejiandaa kushindana, mechi zetu nyingi zimekuwa za ushindani kila tunapokutana lakini dakika 90 zitaamua nani bora, tumefanyia kazi makosa tuliyoyafanya katika mchezo uliopita."


Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema itakuwa mechi nzuri ya kuitazama kutokana na timu zote kuwa na mchezo mzuri na ameiona Azam ikiimarika tofauti na mzunguko wa kwanza.


"Tumetoka kucheza mechi ngumu mfululizo, naamini wachezaji wangu wana uchovu lakini hilo halitaondoa hali ya wao kupambana, wataingia kwa kuwaheshimu wapinzani," alisema na kuongeza;


"Wapo tayari kwa mchezo tunahitaji matokeo ya ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kutetea ubingwa lakini pia natarajia mabadiliko ya kikosi, nitatumia kikosi cha kwanza chote baada ya baadhi kuwapumzisha kwenye mchezo dhidi ya Geita Gold."

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad