Simba inarejea mazoezini kujiandaa na mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri, huku kocha wa zamani wa timu hiyo, Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akilianika faili zima la waarabu akisema anawajulia ndio maana hawakumfunga walipokutana kwenye AFL.
Wekundu wa Msimbazi walikutana na Al Ahly katika mechi mbili za michuano mipya ya Africans Football League ikiwa chini ya Robertinho na kutoka sare ya mabao 3-3, zikifungana 2-2 nyumbani kisha 1-1 ugenini na Wamisri walisonga mbekle nusu fainali kwa kanuni ya mabao mengi ya ugenini.
Timu hizo zitakutana tena katika mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ya kwanza ikipigwa jijini Dar es Salaam Machi 29, kisha kurudiana Aprili 5 na mshindi wa jumla kwenda nusu fainali itakayomkutanisha na mshindi wa mechi ya TP Mazembe ya DR Congo na Petro Atletico ya Angola.
Akiwa anaifuatilia Simba kutokea huko huko kwao Brazili, Robertinho alisema kuwa licha ya Wekundu hao kuwa na changamoto ya ubora wa kikosi, wakijipanga vyema wana uwezo wa kuishangaza Al Ahly aliodai ni kutowapa nafasi ya kukaa na mpira na kuwakaribisha langoni kwako tu.
Kocha huyo aliyewahi kufundisha soka katika nchi za Kenya, Rwanda, Uganda, Tunisia na Angola alisema ni muhimu tu wachezaji wa Simba waelekezwe cha kufanya mapema kama alivyofanya yeye kabla ya kuvaana na Al Ahly mwishoni mwa mwaka jana.
“Nilipokutana na Al Ahly niliwaambia wachezaj hawatakiwi kuwaogopa, ni kweli wao ni timu kubwa lakini hata Simba ni wakubwa ndio maana wapo kwenye Klabu 10 Bora. Pia kama kocha nilikuwa na kazi nzuri ya kuwasoma na baadaye kuja na mpango mzuri wa mechi ndio maana mliona ilibaki kidogo niwaondoe kwao,” alisema Robertinho na kuongeza;
“Hofu yangu ni eneo la ushambuliaji la Simba kwa sasa bado halina watu bora wa kuamua mechi, ni heri wangeamua kubaki na Jean Baleke kuliko hao waliokuja mara nilipoondoka. Kama viungo wa Simba wakipangwa vizuri wanaweza kufanya kitu tofauti kwenye hizo mechi mbili sina wasiwasi na safu ya ulinzi.”
Alisema Al Ahly wanacheza kwa akili na kuwasoma wapinzani wakati wa mchezo ndio maana hubadilika kadri dakika zinavyoenda na hilo alilitambua mapema na kuwabana na kutokubali kupoteza mechi ikiwa ni mara ya kwanza Simba kutoka sare ugenini na nyumbani na wababe hao wa Afrika.
Hata hivyo, Simba ina bahati kwa kuwa na kocha Benchikha anayeijua zaidi Al Ahly kwani alishakutana nayo kwenye CAF Super Cup katikati ya mwaka jana na kuifunga mabao 2-1 wakati akiinoa USM Alger na wachezaji wa timu hiyo walikaririwa na Mwanaspoti kwamba safari hii wanataka kuvuka robo fainali.
Kwa misimu minne kati ya mitano iliyopita tangu Simba iliporejea kwenye mechi za kimataifa, imeishia robo fainali ikiwamo tatu za Ligi ya Mabingwa na moja ya Kombe la Shirikisho Afrika na msimu huu ni mara ya nne kutinga hatua hiyo kwa Ligi ya Mabingwa ikipimana ubavu na Al Ahly iliyowahi kukutana nayo mara nne kwenye mechi za makundi za ligi hiyo na kila moja kushinda nyumbani.