Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete amesema kwa viwango ilivyofikia Simba SC na Young Africans katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika zinaweza kuvuka hatua ya Nusu Fainali.
Akizungumza jijini Dar es salaam kwenye malhojiano na Azam Media, Dk Kikwete amesema kinachohitajika kwa klabu hizo ni kuamini kuwa inawezekana na kujiamini.
“Waamini kuwa inawezekana tukawashinda, Simba SC inapambana na Al Ahly imeshachukua ubingwa mara kadhaa na Young Africans itacheza na Mamelodi Sundowns nayo imeshachukua taji, ni mashindano makubwa makali kweli lakini naamini tunaweza kuvuka na kuwashinda,” amesema.
Kikwete amesema zamani waliamini timu za hapa nchini ni dhaifu lakini kwa sasa mambo yamebadilika kwani tayari zimethibitisha ubora.
“Mchecheto kuwa sisi ni wa mwisho haupo tena, na mimi naamini bado timu zetu zinaweza kushindana na kuvuka hatua inayofuata. Katika vitu ambavyo sina wasiwasi ni hizi mechi, tumefikia hatua ambayo tunaweza kumshinda yeyote, ameongeza.
Katika hatua nyingine, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana amesema Young Africans haiogopi timu kama Mamelodi kwani wamejipanga vizuri kuhakikisha wanashinda.
“Mchezo ni dakika 90 nina hakika viongozi wako katika hali bora zaidi ya kucheza mchezo huo wa marudiano, sina mashaka watatuwakilisha ipasavyo,” amesema
Simba SC itaanza kampeni ya kuitafuta Nusu Fainali Ijumaa (Machi 29) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na Young Africans Machi 30 ambapo zitakwenda kurudiana ugenini Misri na Afrika Kusini Aprili 5, mwaka huu.