Maswali 9 Yenye Utata ya Mo Dewji Kuinunua Simba

Maswali 9 Yenye Utata ya Mo Dewji  Kuinunua Simba


Wakati Simba ikiendelea kujipanga kwa ajili ya mechi itakayoamua hatima yake kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kesho Jumamosi dhidi ya Jwaneng Galaxy kutoka Botswana, rais wa heshima wa klabu hiyo, Mohammed Dewji 'Mo' ametoa kauli iliyozua sintofahamu baada ya kudai ameinunua Simba miaka mitano iliyopita.


Dewji alisema hayo kwenye mahojiano katika kipindi cha 'Ahmad Mahmood Show'kinachoruka katika mitandao tofauti ikiwemo Youtube, na Alhamis, Februari 29, 2024 katika ukurasa rasmi wa mtandao wa Instagram wa Mo Dewji alichapisha kipande cha video hiyo akieleza kuinunua Simba huku akiweka wazi ndio uwekezaji mkubwa kwake.


Mo alisema: "Nadhani kitu ghali zaidi nilichowahi kununua ni klabu ya mpira. Inaitwa Simba, ina mashabiki 35 milioni. Niliinunua hii klabu miaka mitano iliyopita. Nimepoteza kama Dola 4 milioni (takriban Sh10.2 bilioni) kwa mwaka mmoja na kwa miaka mitano iliyopita nimepoteza Dola 20 milioni (sawa na Sh51 bilioni)"


Aliongeza kuwa, "lakini nimeifanya Simba kuwa katika klabu 10 bora Afrika, ni jambo jema kwani limeleta furaha kwa watu na nina furaha na hilo."


Mo alipoulizwa kuhusu kupata faida kupitia timu hiyo, alisema kwa sasa hapati , lakini anatumaini baadaye ataanza kupata mkwanja kutokana na umiliki wake.


"Nadhani kwa sasa soka la Afrika bado lipo chini ukilinganisha na maeneo mengine, lakini nadhani ni suala la muda. Soka la Afrika litakuwa sawa na maeneo mengine duniani," alisema na kuongeza:


"Lakini kwa sasa naendelea kupoteza pesa na natumaini kuwekeza katika vijana na labda kwa baadaye nitapata faida ila kwa sasa nafanya matangazo ya bidhaa zangu kupitia klabu lakini yote kwa yote bado ni jambo la gharama na napoteza pesa."


Kauli hiyo imezua sintofahamu na kuwashtua wanachama wa klabu hiyo, mashabiki na wadau wa soka nchini kutokana na taarifa rasmi ya mwisho ya klabu kupita kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria wa Simba, Wakili Hussein Kitta aliyoitoa Januari 18, mwaka huu kuwa kama wanachama watapitisha maboresho ya rasimu ya katiba ya klabu hiyo, mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa Simba utafanikiwa ndani ya muda mfupi, tofauti na ambavyo ulikwama kwa miaka mitano iliyopita.


Taarifa hiyo iligongelewa msumari na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro aliyesema wizara haijapitisha katiba ya Simba, hivyo timu hiyo ifuate na kuheshimu sheria.


"Wizara haijapitisha katiba ya Simba. Katiba hiyo ilikuwa na upungufu na ilikiuka sheria za ushindani wa haki, Rita na BMT," alisema Ndumbaro.


Kulingana na taarifa hizo, ni dhahiri taarifa ya Mo Dewji kuinunua Simba inachanganya na yafuatayo ni maswali tisa ya kujiuliza juu ya jambo hilo:


1. NANI ALIMUUZIA TIMU?


Hili ndilo swali la kwanza kujiuliza kwani Simba kabla ya kauli hiyo inafahamika kuwa ni timu ya umma ikimilikiwa na wanachama, hivyo ni nani alimuuzia Mo Dewji, lini na wapi?


2. ALIINUNUA KIASI GANI?


Swali lingine la kujiuliza ni kiasi gani kilitumika kuinunua Simba? Tenda ya mauzo au manunizi ilitangazwa wapi ikiwahusisha kina nani? Je hakukuwa na ushindani? Wanachama walipitisha lini kuiuza klabu yao?


3. ZILE SH20 BILIONI ZA NINI?


Kama Mo aliinunua Simba miaka mitano iliyopita kwanini mwaka 2021 alitoa hundi ya Sh20 bilioni kwa Simba zilizokuwa malipo ya asilimia 49 ya hisa ambazo anapewa mwekezaji katika mfumo wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo? Zile pesa zilikuwa za nini? Je kweli alizitoa?


4.MBONA WANACHAMA WANAKUTANA?


Mo Dewji anadai kuinunua Simba, lakini katika Mkutano Mkuu wa klabu hiyo hakuonekana uliofanyika hivi karibuni. Kwanini uamuzi wote katika mkutano huo ulifanywa na wanachama na wapo kama kina nani katika umiliki wake kwa klabu hiyo?


5. SIMBA, SERIKALI NI WAONGO?


Kama kweli mo kainunua kitambo Simba mbona klabu hiyo na Serikali (kwa kuzingatia ndiye msimamizi wa haki za umma) hawakuweka wazi mauzo ya klabu hiyo? Mbona Simba na Serikali zinaeleza mchakato wa mabadiliko ya katiba na uendeshaji unaendelea na haujakamilika? Je pande hizo ni waongo?


6. SH51 BILIONI ZIMEPOTELEA WAPI?


Mo katika mahojiano hayo ameeleza amepoteza Dola 20 milioni (sawa na Sh51 bilioni) kwa Simba. Hizo pesa amezipotezea wapi na Kwenye nini? Nani au chombo gani huru kilichothibitisha upotevu au hasara hiyo?


7. MBONA KALALAMIKA KARIBUNI?


Miezi michache iliyopita, Mo alidai kucheleweshwa kuwekeza ndani ya klabu hiyo, je ni nini alichokuwa analalamikia? Ni uwekezaji au umiliki wa klabu hiyo?


8. KWANINI SASA?


Mo amedai kuinunua klabu hiyo miaka mitano iliyopita kwanini sasa ndio anasema ameinunua Simba? Miaka mitano yote alikuwa wapi kuuhabarisha umma juu ya hili?


9.SIMBA INASEMAJE?


Kama Mo ameinunua Simba na mmiliki wa klabu hiyo kwa miaka mitano sasa, Simba yenyewe inasemaje?


Mwanaspoti imewatafuta viongozi mbalimbali wa Simba kuzungumzia jambo hilo, lakini hakuna hata mmoja aliyetoa ufafanuzi huku baadhi yao wakisisitiza kuwa kwa sasa wanachoangalia zaidi ni mechi dhidi ya Jwaneng Galaxy inayopigwa keho. Pia hakuna ukurasa rasmi wa Simba uliochapisha jambo hilo.


WASIKIE WADAU


Miongoni mwa wanachama maarufu wa Simba waliozungumzia suala hilo ni Hamis Kilomoni na hapa anasema kwamba klabu huyo iliyoanzishwa mwaka 1936 haijauzwa kwa mtu yeyote, bali inawafadhili na wadhamini.


"Timu haijauzwa na haiwezi kuuzwa hovyo. Watu wanakuja kuidhamini na kufadhili klabu, lakini hakuna hata mmoja aliyeuziwa wala kuinunua klabu hii. Msidaganywe," anasema Kilomoni.


John Komba, mwanachama wa Simba anasema anaamini timu hiyo bado haijauzwa na kauli ya Mo Dewji ni mwendelezo wa kauli alizodai kuwa sio rasmi juu ya timu yao.


"Simba haijauzwa na ingeuzwa wanachama tungejulishwa kwenye mkutano mkuu. Kauli za Mo Dewji inabidi mzizoee japo sijui huwa anafikiria nini kusema hivyo, lakini ninachojua Simba haijauzwa na kinachoendelea ni mchakato wa mabadiliko ambao hata hivyo bado haujakamilika," anasema Komba.


Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali anasema hawezi kuzungumzia hilo na kuelekeza atafutwe mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah 'Try Again' ambaye jitihada za kumpata ziligonga mwamba.


Upande wa Serikali, alipotafutwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo Taifa (BMT), Neema Msitha alisema hawezi kuzungumzia jambo hilo kwani sio rasmi, huku simu ya mwenyekiti wa Simba, Murtaza Ally Mangungu ikiita bila kupokewa

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad