Mwili wa Beatrice Wazikwa Mara ya Pili, Mtuhumiwa Kupandishwa kizimbani

Mwili wa Beatrice Wazikwa Mara ya Pili, Mtuhumiwa Kupandishwa kizimbani


Mwili wa Beatrice Ngongolwa (32), umezikwa kwa mara ya pili nyumbani kwao katika Kijiji cha Magunga, Wilaya ya Iringa vijijini huku mtuhumiwa wa mauaji Mohamed Salanga (37) akitarajiwa kufikishwa mahakamani kesho.


Beatrice anadaiwa kuuawa kwa kipigo na Salanga, usiku wa Desemba 31 mwaka jana kisha mwili wake kuzikwa ndani ya nyumba waliyokuwa wakiishi, Kijiji cha Skutari, Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro.


Tukio hilo lilibainika Machi 21, 2024 na Jeshi la Polisi likiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamud Shaka walikwenda kuufukua mwili wa Beatrice, Machi 22 2024 na kuupeleka Hospitali ya Rufaa ya Morogoro.


Leo Jumatatu, Machi 24, 2024, Calius Ngongolwa anayeishi mkoani Iringa alikabidhiwa mwili wa mwanaye na kuzikwa.


Baba huyo amesema pamoja na binti yake kuuawa kikatili lakini kitu kingine kinachomuuma ni kukaa zaidi miaka miwili bila ya kuwasiliana naye ambaye ni mtoto wa pili katika familia yake.


Amesema yeye kwa asili ni Muhehe anatokea mkoani Iringa lakini maisha yake na familia yake kwa miaka mingi ipo mkoani Kilimanjaro, hivyo mara ya mwisho kuonana na binti yake ilikuwa mwaka 2022, Kilimanjaro.


Ngongolwa amesema baada ya hapo hakuweza kumuona wala kuwasiliana naye tena hadi Machi 23, 2024 alipopigiwa simu na polisi kuwa binti yake ameuawa na kufukiwa ndani.


"Tangu alipomaliza shule ya msingi mwaka 2005 mkoani Kilimanjaro, Beatrice alikuwa akijishughulisha na ujasirimali na hapo ndipo alipopata kijana mmoja na akazaa naye mtoto wa kwanza wa kike na baadaye walishindwana na akapata mwanamume mwingine ambaye alizaa naye watoto wawili wa kiume," amesema Ngongolwa.


Hata hivyo, amesema mtuhumiwa hakuwa mume wa binti yake na wala hakuzaa naye isipokuwa walikuwa wakiishi tu na katika kipindi chote walichoishi hakuwahi kusikia madhira wala mateso aliyokuwa akiyapata binti yake na hakujua kama yupo Kilosa anaishi na mtuhumiwa huyo.


Akieleza namna binti yake alivyokutana na mtuhumiwa, Ngongolwa amedai mtuhumiwa huyo aliwahi kufungwa miaka minane jela na wakati huohuo mwanamume wa Beatrice naye alifungwa miaka miwili Gereza la Karanga lililopo mkoani Kilimanjaro na wote walimaliza kifungo chao mwaka 2022.


Alisema wakiwa magereza mtuhumiwa na mwanamume wa Beatrice walikuwa marafiki na hata baada ya kumaliza kifungo mwanamume wa Beatrice alimchukuwa mtuhumiwa Salanga na kwenda kuishi naye nyumbani kwake pamoja na Beatrice na wakiwa nyumbani hapo mtuhumiwa alianza uhusiano ya kimapenzi na Beatrice.


"Mwenzake alimkaribisha nyumbani ili aweze kujitafuta na apate pesa za kurudi kwao Singida, lakini alitumia mwanya huo akaanzisha uhusiano na Beatrice, baadaye mwanamume wa Beatrice alikwenda kijijini kwao Sanya Juu kutafuta vibarua ili akipata amwite rafiki yake (mtuhumiwa) wakafanye," amesema Ngongolwa.


"Akiwa huko kijijini kwao huku nyuma mtuhumiwa Salanga alimtorosha Beatrice pamoja na watoto wake na kwenda kuishi naye Kilosa na tangu hapo hakupatikana kwenye simu wala hakurudi tena Moshi, mpaka juzi nilipopigiwa simu na kuelezwa kuwa ameuawa na huyo bwana ambaye Mimi wala simfahamu,"amesema.


“Huyu mtuhumiwa baada ya kuoneshwa pale polisi nilimkumbuka na namfahamu vizuri kwa sababu akiwa anaishi pale nyumbani kwa binti yangu na mwanamume wake niliwahi kumuona na pia aliwahi kuja nyumbani kwangu kama mara tatu kutembea akiwa na mwanamume wa Beatrice."


Amesema katika kipindi chote alichopotea binti yake kama familia ilifanya jitihada mbalimbali za kumtafuta lakini hawakufanikiwa kumpata hata hivyo waliamini yuko hai isipokuwa ni hali ngumu ya utafutaji ndio inayomfanya aondoke Kilimanjaro.


Kuhusu uchunguzi wa mtuhumiwa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema mwili huo ulikabidhiwa kwa baba yake baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kidaktari na taarifa ya uchunguzi huo itakuwa ni sehemu ya ushahidi mahakamani.


Amesema baada ya kugundulika kwa mauaji hayo haraka Jeshi la Polisi lilianza uchunguzi wake na baadaye lilipeleka jalada kwenye ofisi ya mwanasheria mashitaka mkoa, ambaye yeye ndio mwenye wajibu wa kuandaa hati ya mashitaka kulingana na taarifa ya uchunguzi tulioufanya.


Amesema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kesho asubuhi kwa kuwa tayari maandalizi yote ya kumfikisha huko yamekamilika.


Kuhusu malezi ya watoto watatu walioachwa na Beatrice, mmoja akiwa na miaka 11, wengine tisa na wa mwisho minne, babu yao amesema bado wapo chini ya uangalizi wa Serikali na baada ya kumaliza shughuli za mazishi atarudi mkoani Morogoro kukaa na viongozi wa Serikali ya Kilosa pamoja na Polisi kwa ajili ya kujua wapi watoto hao watakapoishi.


Amesema yeye yuko tayari kulea wajukuu zake na katika kikao hicho na Serikali amepanga kuwaomba wamkabidhi wajukuu zake kwa kuwa ndio faraja yake iliyobaki.


"Nikishamaliza taratibu za mazishi nitarudi Moshi lakini itabidi kwanza nishuke Morogoro ili niweze kukutana na viongozi wa Serikali na kuzungumza nao na nitawaomba niondoke na wajukuu zangu na nitawalea mwenyewe," amesema Ngongolwa.


Akizungumza maisha ya watoto watatu wa marehemu Beatrice, Mkuu wa wilaya ya Kilosa ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya amesema kuwa watoto hao kwa sasa bado wapo chini ya uangalizi wa Serikali kupitia maofisa ustawi wa jamii ambao wamekuwa wakiwapa nasaha.


"Ni kweli baba wa marehemu ameshakuja Morogoro kuchukua mwili wa binti yake kwa ajili ya kwenda kuzika kwao Iringa lakini ushauri tulioupata kutoka Kwa wataalamu wa saikolojia ambao ni maofisa ustawi, tumeona watoto hawa waendelee kuwa kwenye uangalizi wa wataalamu hao ambao wamekuwa wakiwapa nasaha ili kuwarudisha kwenye hali nzuri, kiukweli hawa watoto wameathirika kisaikolojia," amesema Shaka.


Pia, amesema baada ya watoto hao kukaa sawa kisaikolojia ndipo watakapoangalia namna ya kuwarudisha shule ili waendelee na masomo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad