Raha iliyoje kutazama mpira Ulaya. Unachukua treni katikati ya jiji la Madrid kuelekea nje kidogo ya mji kwenye Uwanja wa Wanda Metropolitano. Nyumbani mwa Atletico Madrid. Njiani mashabiki karibu wote wamevaa jezi za Atletico Madrid.
Tukifika uwanjani tunaingia kistaarabu. Tunakunywa bia baridi na kula soseji. Pambano ni dhidi ya Liverpool. Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Mashabiki wachache wa timu nyingine wanaoonekana ni wa Liverpool. Wamewekewa jukwaa lao dogo. Vinginevyo ni raha tupu. Hakuna shabiki hata mmoja wa Real Madrid. Akafanye nini katika pambano la Atletico Madrid na Liverpool.
Aharibu nauli yake, muda wake, kiingilio chake kwenda kutazama pambano lisilomuhusu? Hapana! Anakaa nyumbani. Wakati mwingine hata katika televisheni haangalii. Anaendelea na kazi zake au starehe zake. Na ndivyo yalivyo maisha ya mashabiki wengi karibu dunia nzima.
Afrika Kusini shabiki wa Kaizer Chiefs hawezi kujisumbua kwenda kutazama mechi za Orlando Pirates. Zinamuhusu nini? Shabiki wa Zamalek hana muda wa kwenda kutazama mechi za Al Ahly. Zinamuhusu nini? Ni kweli anataka Simba imfunge Al Ahly pale Cairo siku chache zijazo lakini hana muda wa kutafuta jezi ya Simba wala kwenda kuishangilia.
Kama Basi la Simba litapita mbele yake atalishangilia na kuwatakia mema. Halafu basi. Matokeo atayasikia katika taarifa ya habari kwenye televisheni. Au kama ana marafiki zake mashabiki wa Al Ahly basi anaweza kutazama nao mechi huku akinywa kahawa na kufurahi kama wanaelekea kupoteza mechi hiyo ya soka.
Kwa wenzetu ukiona shabiki kaenda mechi ya mtani dhidi ya timu nyingine basi huenda akawa amemsindikiza mgeni au rafiki yake. Kwamba anampa kampani tu kwa sababu hajui mipangilio ya kwenda uwanjani au namna ya kuingia au mengineyo. Huwa inatokea mara chache. Mgeni wako ni Manchester United wewe ni Manchester City. Utamsindikiza tu bila ya kuvaa ya City wala kupiga kelele.
Soka ni utamaduni. Maili nyingi kutoka kwao kuna nchi huku inaitwa Tanzania. Tuna utamaduni tofauti. Bahati mbaya hakuna kitu kibaya kama kufuta utamaduni. Unawezaje? Hakuna namna. Achilia mbali kuombea hadharani lakini kuna mashabiki wanakwenda uwanjani kabisa kushangilia timu pinzani dhidi ya mtani. Ndio maisha ambayo tumeyachagua.
Utamaduni wa kwanza uliozidisha chuki hizi ni ukweli kwamba nchi nzima imegawanyika katika pande mbili. Simba na Yanga basi. Afadhali kila shabiki angekuwa anapenda timu ya kwao. Dodoma, Mtwara, Mwanza, Tabora na kwingineko. Lakini hapana. Kila mtu, nchi nzima anapenda Simba au Yanga. Sijawahi kuona popote duniani zaidi ya Tanzania.
Kwanini uende katika mechi ya mtani? Inashangaza kidogo. Na kitu kibaya zaidi ni kwamba tiketi zinauzwa katika mfumo wa kushangaza. Kwa wenzetu tiketi zinauzwa na klabu na zinauzwa kwa ajili ya mashabiki wao tu. Chache zinapelekwa kwa ajili ya mashabiki wa timu wanayocheza nayo. Sisi tiketi zinauzwa na Shirikisho. Zinauzwa kwa yeyote yule anayetaka kwenda uwanjani. Shida inaanzia hapo.
Ni utamaduni tu kwamba unakwenda unatoka nyumbani, unatumia nauli yao, kiingilio chako, muda wako, kwa ajili ya kwenda kuizomea Simba dhidi ya Al Ahly au kuizomea Yanga dhidi ya Mamelodi. Sidhani kama kuna ambacho tunaweza kufanya kuzuia hilo. Hakuna jambo gumu kama kuzuia jambo hilo.
Majuzi rafiki yangu, kaka yangu, Waziri wa Wizara ya mambo haya, Damas Ndumbaro alijiingiza katika vita ambayo hawezi kushinda. Kutaka watu wawe wazalendo kwa hizi timu za Simba na Yanga. Haiwezekani. Sehemu pekee ambayo Watanzania wanaweza kukutana katikati ni katika Taifa Stars tu. Basi. Huku kwa Simba na Yanga ni ngumu.
Yanga akimfunga Mamelodi anayepata shida sio shabiki wa Mamelodi. Anapata shida shabiki wa Simba ambaye hata mechi ilikuwa haimuhusu. Simba akimfunga Al Ahly anayepata shida ni shabiki wa Yanga ambaye mechi ilikuwa haimuhusu kabisa. Haishangazi kuona mashabiki wanakwenda kushangilia wapinzani. Wengine wanaenda mbali zaidi kwa kwenda kupokea timu Airport.
Najua kwamba Simba na Yanga wanaombeana mabaya. Sijui ilianzia lini lakini kwa umri wangu chuki kubwa zaidi iliendelezwa katika lile pambano la fainali za CAF mwaka 1993. Simba dhidi ya Stella Abidjan. Mgeni rasmi alikuwa Mzee Rukhsa. Mwenyezi Mungu amrehemu. Kabla ya mechi nchi nzima ilikuwa imesisitiziwa kwamba tunapaswa kuwa wazalendo kwa sababu Simba walikuwa wanakaribia kutuletea kombe la kwanza kubwa nchini.
Mfumo wa tiketi ulikuwa huu huu kwahiyo hakukuwa na namna ya kuweza kuwazuia Yanga kuingia uwanjani. Ujumbe tu kutoka kwa Rais na watu wazito ni kwamba Yanga walipaswa kuishangilia Simba. Walipokuja uwanjani hawakuishangilia Simba wala Stella lakini Boli Zozo alipoifungia Stella bao la pili na kufanya matokeo kuwa 2-0 ndipo Yanga walipolipuka na kuimba kwa furaha wakisema “uzalendo umetushinda”.
Kuanzia hapo kila kitu kimekuwa wazi. Hakuna unafiki tena. Na umekuwa mwendo wa visasi kiasi kwamba katika dunia hii ya utandawazi watu wamekuwa wakivaa hadi jezi za timu pinzani. Si zinauzwa nchini na watu wanalipa kodi kuziingiza? Hakuna tunachoweza kuzuia kwa sasa. Afadhali tungezuia huko mwanzoni kwa kukemea mambo kadhaa.
Na sasa nadhani imekuwa kama chachu tu kwa timu zetu kufanya vizuri. Ukiwafunga Mamelodi unawafunga mdomo Mamelodi na Simba. Ukiwafunga Al Ahly unawaziba midomo Al Ahly na Yanga. Ni kazi ngumu lakini lazima wachezaji wetu waifanye. Hakuna namna kwa sababu hakuna tunachoweza kubadili kama Dk. Ndumbaro alivyosema na baadaye kutolewa taarifa rasmi kwamba “alitania tu.”
Acha mashabiki waende uwanjani kushangilia wapinzani. Kitakachowanyamazisha ni ubora tu wa timu ya nyumbani. Unadhani Yanga walifurahi kuona Simba wanakwenda robo fainali mara nne mfululizo? Ubora wa Simba ya Jose Luis Miquissone yule na wahuni wenzake uliwalazimisha. Baadaye wenyewe walichoka kwenda kushangilia wapinzani wa Simba.
Ni hadithi ya Yanga kufika fainali za Shirikisho. Watu walioumia zaidi duniani ni Simba lakini hawakuwa na la kufanya. Ubora wa Yanga na kina akina Aziz Ki uliwalazimisha. Huu ndio ukweli halisi. Ukweli ambao lazima usemwe.
Na sasa kazi hii tuikabidhi kwa kina Clatous Chama na Pacome Zouzoua. Wao ndio wanaweza kutuondolea mashabiki wa mtani uwanjani. Waifanye kazi yao kwa ufasaha tu. Simba haiwezi kufungwa na Al Ahly kwa sababu ya mashabiki 30 wa Yanga waliojitokeza kuishangilia Al Ahly Kwa Mkapa.