Jeshi la Polisi nchini Tanzania limeanza uchunguzi kuhusu tukio la Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka ambaye gari lake lilishambuliwa kwa risasi na yeye akiwemo ndani pamoja na dereva wake lakini hawakupata madhara.
Tukio hilo lilitokea jana Ijumaa Machi 29, 2024 katika kijiji cha Ngabolo wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara wakati Ole Sendeka akiwa safarini kutoka Dodoma kwenda jimboni kwake Simanjiro mkoani humo.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Machi 30, 2024 na Msemaji wa Polisi Tanzania, David Misime imeeleza: Jeshi limepokea taarifa ya mbunge wa Simanjiro, Ole Sendeka na dereva wake wakiwa safarini gari walililokuwa wanatumia kushambuliwa kwa risasi kwa bahati nzuri hakuna aliyepata madhara.”
Misime amesema: “Polisi wanafuatilia tukio hilo kwa ukaribu sana na uchunguzi umeshaanza baada ya kupokea taarifa, timu ya watalaamu wa uchunguzi inayohusisha matumizi ya risasi kutoka makao makuu ya Polisi Dodoma imetumwa kushirikiana na timu ya mkoa wa Manyara kuchunguza kwa kina tukio hilo ili kubaini waliohusika kina nani au kusudio lao ni nini."
Amesema baada ya uchunguzi huo, baada ya uchunguzi huo wa wataalamu, taarifa kamili itatolewa.
Jana Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Lucas Mwakatundu akizungumza na Mwananchi Digital alisema: "Ole Sendeka akiwa na dereva wake na gari lao walishambuliwa kwa risasi ila hawakudhurika.”
Kamanda Mwakatundu amesema polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na hakuna mtu anayeshikiliwa kutokana na tukio hilo.