MSHAMBULIAJI Prince Dube ameingia Uwanja wa Benjamin Mkapa saa moja kabla ya pambano la Ligi Kuu Bara kati ya mechi ya ligi kati ya Azam FC na Yanga kupigwa uwanjani hapo, huku akiwa amesindikizwa na mabaunsa wawili.
Dube mwenye mabao saba katika Ligi Kuu kwa msimu huu, Machi 7 mwaka huu kupitia ukurasa wa mtandao wa instagram alitangaza kuachana na Azam aliyoitumikia kwa misimu minne, mara baada ya kufika uwanjani hapo moja kwa moja alienda kukaa katika Jukwaa la VIP B, huku mabaunsa wakibaki wamesimama kumlinda.
Staa huyo ana mvutano na klabu ya Azam kutokana na uongozi kutoa taarifa kuwa, Dube bado ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu na Wanachamazi hao, hivyo anapaswa kufuata taratibu za kuvunja mkataba ili kuwa huru ikiwamo kulipa Dola 300,000 (zaidi ya Sh 700 milioni).
Hata hivyo, Azam iliweka wazi kumweka sokoni Dube huku ikitanabaisha tayari imepokea ofa mbili kutoka kwa Simba na Al Hilal ya Sudan lakini bado inakaribisha ofa nyingine zaidi, huku akihusishwa na Yanga inayoelezwa ni klabu anayoipenda kwani amekuwa akiifuatilia ikicheza kama ilivyotokea siku ya pambano la makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad na Yanga kushinda 4-0.
Dube raia wa Zimbambwe ndiye aliyekuwa kinara wa mabao wa Azam kabla ya kuamua kuachana na timu hiyo hivyo leo atakaa jukwaani akiwashuhudia wenzake wakicheza na Yanga.
Katika eneo alilokuwa akicheza Dube, kocha wa Azam Youssouf Dabo leo amempanga Abdul Suleiman 'Sopu'.