Rais Samia : Maktaba Yangu Imeungua Moto



RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kifo cha Rais wa Pili wa Tanzania, Alhaji Ali Hassan Mwinyi ni pigo kwake binafsi na taifa kutokana na mambo makubwa aliyofanya kiongozi huyo kitaifa na kimataifa.

Amesema kifo cha Rais Mwinyi, maarufu Mzee Rukhsa, ni sawa na kuungua moto kwa maktaba kubwa iliyosheheni vitabu vya maarifa.

"Kifo chake ni pigo kwa taifa na kwangu binafsi kama Mkuu wa Nchi. Nimeukumbuka msemo wa kiafrika unaosema 'anapofariki mzee, maktaba huungua moto', yaani kila kitu alichonacho mzee, akifariki dunia ni kama maktaba iliyoungua moto. Kumbukumbu zote zinapotea," Rais Samia amesema katika salamu zake wakati akiongoza wananchi kuaga mwili wa Mzee Rukhsa kwenye Uwanja wa Amani, Unguja jana.

"Mtakubaliana nami kwamba maktaba yetu kubwa iliyosheheni hadithi nyingi nzuri imeungua moto. Mzee Mwinyi alikuwa maktaba inayotembea iliyosheheni vitabu vyenye mafunzo mengi ya uadilifu, uzalendo, ustahimilivu, ujasiri, unyenyekevu, uchamungu na mambo mengi mengine.

"Msiba huu ni wetu sote, ni msiba wa taifa, ila ni msiba mzito zaidi kwa familia kwa kuondokewa na nguzo yao.

"Mbuyu umeanguka. Kwa niaba ya wananchi wa Tanzania, ninatoa pole kwa familia, ninatoa pole kwa Mama Sitti, Mama Khadija, watoto wa marehemu wakiongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, wajukuu na vitukuu kwa kuondokewa na mpendwa wao. Tambueni kuwa pigo hili ni letu sote," alisema.

Rais Samia alisema nchi imepoteza kiongozi mwenye historia kubwa kitaifa, Afrika Mashariki na Bara la Afrika kwa ujumla, akimtaja alipenda nchi yake na aliitumikia kwa moyo na kuivusha katika kipindi kigumu kuanzia alipokuwa Rais wa Zanzibar na baadaye Rais wa Tanzania (1985-1995).

"Ingawa tuna simanzi kwa kuondokewa na mzee wetu, tuna faraja kwamba tumemuenzi na kumpa maziko ya kitaifa na kumwombea dua njema," Rais Samia alitia moyo waombolezaji.

Alisema Mzee Mwinyi alikuwa mcha Mungu aliyeishi maagizo ya Mwenyezi Mungu na alitii miongozo ya Dini ya Kiislamu, akiwashukuru wananchi na viongozi wa dini kwa kuungana na serikali kuomboleza kifo cha kiongozi huyo.


Rais Samia pia alishukuru wakuu wa nchi jirani na rafiki waliotuma wawakilishi kushiriki mazishi hayo.

Nchi zilizotuma wawakilishi wake Zanzibar kushiriki mazishi hayo ni Burundi, Namibia na Comoro.

Rais Samia alisema Mzee Mwinyi alipitia kipindi kigumu katika uongozi wake kwa kuwa alichukua 'kijiti' toka kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere ikiwa katika hali mbaya kiuchumi, lakini alihakikisha nchi na wananchi wanakuwa na utulivu.


Alisema kuwa kipindi hicho kulikuwa na uhaba wa fedha za kigeni na bidhaa muhimu, Mzee Mwinyi akibadili sera na kutoa rukhsa ya biashara huria nchini.

Rais Samia pia alimtaja Mzee Rukhsa ni kiongozi wa mfano katika kupenda haki na kutenda haki. Jambo ambalo Rais Mwinyi amelisisitiza katika wosia wake kwa viongozi uliomo katika sura ya mwisho ya kitabu chake cha 'Mzee Rukhsa, Safari ya Maisha Yangu'.

Rais Samia alimtaja Mzee Rukhsa alikuwa mpenda demokrasia, akiruhusu kusikika sauti tofauti na zilizozoeleka kusikika serikalini, pia vyombo vya habari vya watu binafsi na taasisi ambazo ziliikosoa serikali.

"Mzee Mwinyi ndiye aliyeruhusu uwekezaji binafsi, zikiwamo kampuni za simu. Alama zake zimeendelea kufuatwa na serikali zilizofuata.

Mzee Mkapa, kwa mfano alipata pa kuanzia kuomba IMF kuifutia madeni Tanzania," alisema.

ALICHOCHOTA

Rais Samia, akiorodhesha mambo muhimu aliyojifunza kutokana na maisha na uongozi wa Mzee Mwinyi, amtaja alikuwa mwanageuzi asiyeyumba.

Alisema kuwa hadi mwaka 1985 serikali ilikuwa haijakubaliana na Sera mpya za uchumi zilizotangazwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), lakini kuingia madarakani kwa Mzee Rukhsa kulibadili mtazamo kiuchumi.

NASAHA ZA JANABI

Rais Samia aliahidi kuyaenzi maisha ya Mzee Rukhsa kupitia mambo makuu matatu ambayo ni kusimamia kikamilifu ustawi wa wananchi kwa kushamilisha sekta binafsi, kusimamia haki na kuwa na subira na ustahimilivu.

“Pia nitamkumbuka kwa kuishi misingi bora ya maisha katika maisha yake yote. Ninakumbuka tukiwa kwenye matembezi ya husani katika Kampeni ya Afya Yangu Mtaji Wangu', tuliongozwa na Mzee Mwinyi na mara zote alikuwa anaongoza halafu anakwenda ananisubiri nunamfuata, ikabidi aanze kunifuata mimi lakini baada ya muda kanipita tena kuonesha alivyokuwa imara,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Rais Samia alisema kuwa waandishi wa habari walimfuata Mzee Mwinyi kumhoji wakitaka kujua siri ya kuishi miaka mingi akiwa imara, naye aliwajibu kuwa "ni mazoezi", lakini siri ya pili kwa vijana wa kiume wamfuate pembeni awaelezee vyema.

Kauli hiyo ya Rais iliibua kicheko msibani, waombelezaji witabasamu kwa sekunde chache kwenye Uwanja wa Amani kisha kuendelea kusikiliza salamu za Rais Samia.

Mkuu wa Nchi aliendelea kusema kuwa kupitia Hayati Mwinyi, lipo fundisho la kuwa na uwezekano wa kujifunza mambo ukubwani na kuyatilia maanani, akimwelezea alivyoendelea kuishi na misingi hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi ya kutembea kilomita tano kila siku alipokuwa na umri wa umri wa miaka 50 na kutenga nusu saa kuendesha baiskeli jioni.

“Alifanya hivyo ili kuwatia ari wananchi kufanya mazoezi kwa kuwa ni njia kujiimarisha na kujilinda dhidi ya magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza kama vile kisukari na presha na ni matumaini yangu sote tutajifunza kitu kuhusu mazoezi kwa kuanza na kuwa na nidhamu. Ninadhani hapa Prof.Janabi naye anaendeleza wosia huo,” alisema Rais Samia na kuibuka kicheko tena miongoni mwa waombolezaji.

Katika kitabu chake cha 'Mzee Rukhsa, Safari ya Maisha Yangu', Mzee Mwinyi anaeleza kwa kina namna alivyopokea kijiti kutoka kwa Mwalimu Nyerere, nchi ikiwa imetengwa na 'dunia' kiuchumi. Moja ya hatua alizochukua ni kukubaliana na masharti ya IMF, kupunguza idadi ya watumishi kwenye mashirika na taasisi za umma na hata kuyafuta baadhi ya mashirika.

Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ni miongoni mwa taasisi zilizokumbwa na uamuzi wa kupunguziwa watumishi, Mzee Rukhsa akisema kwenye kitabu chake kuwa alilazimika kuwafuta kazi watumishi wa kampuni hiyo na kufunga baadhi ya ofisi za kampuni hiyo katika nchi mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad