Droo ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika inatarajiwa kuchezeshwa leo kuanzia saa 10:00 jioni kwa muda wa Afrika Mashariki, huko Cairo, Misri.
Timu mbili zinazoiwakilisha Tanzania kwenye mashindano hayo, Yanga na Simba zitafahamu wapinzani wao katika hatua ya robo fainali kupitia droo hiyo ambayo itaendeshwa na kusimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Kutakuwa na vyungu viwili katika uchezeshaji wa droo hiyo ambapo cha kwanza kitakuwa na timu nne ambazo zimemaliza katika nafasi ya pili kwenye makundi wakati nyingine nne zitakuwa katika chungu cha pili ambacho kina timu zilizomaliza zikiwa kinara kwenye makundi.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, timu zilizomaliza katika nafasi ya pili haziwezi kukutana katika hatua ya robo fainali kama ilivyo kwa zile zilizomaliza katika nafasi ya kwanza ingawa zinaweza kuumana kwenye nusu fainali au fainali na ifahamike kwamba, timu zilizokuwa kundi moja haziwezi kukutana kwenye robo fainali.
Kwenye hatua hiyo ya robo fainali, pia timu zilizomaliza katika nafasi ya pili kwenye hatua ya makundi zitaanzia nyumbani kwenye hatua hiyo ya robo fainali na zitamalizia ugenini.
Chungu cha kwanza kitakuwa na timu za Simba, Yanga, Esperance na TP Mazembe wakati chungu cha pili kikiwa na Al Ahly, Petro Luanda, Mamelodi Sundowns na Asec Mimosas.
Kwa kushika nafasi ya pili kwenye kundi B, Simba inaweza kupangwa na mojawapo kati ya Mamelodi Sundowns, Al Ahly au Petro Luanda wakati Yanga iliyomaliza ikiwa nafasi ya pili kwenye kundi D inaweza kukutana na ama Petro Luanda, Mamelodi Sundowns au Asec Mimosas.
Timu tatu ambazo mojawapo inaweza kukutana na Simba, zimeonekana kuwa moto wa kuotea mbali kila moja katika mechi ambazo kila moja imecheza baada ya kujihakikishia tiketi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mamelodi tangu ilipokata tiketi ya robo fainali, imecheza mechi tisa za mashindano tofauti ambapo imeshinda michezo mitano na kutoka sare nne, ikifunga mabao 18 na yenyewe imeruhusu mabao mawili tu wakati Petro Luanda katika mechi nne ilizocheza baada ya kujihakikishia kufuzu, imepata ushindi mara tatu na kutoka sare moja, ikipachika mabao nane na haijafunga bao lolote.
Al Ahly yenyewe baada ya kutinga robo fainali ilicheza mechi tano, ikaibuka na ushindi mara zote, ikifunga mabao tisa na nyavu zake kuguswa mara moja.
Asec Mimosas inayoweza kukutana na Yanga, imeonekana kuwa nyanya tangu ilipofuzu ambapo baada ya hapo, imepata ushindi mara moja tu katika mechi tano, imetoka sare moja na kupoteza tatu, ikifunga bao 1 na imefungwa mabao mawili.
Akizungumzia robo fainali hiyo, nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto alisema kuwa wapo tayari kupambana na timu yoyote ambayo watapangiwa nayo katika michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu.
“Tumejiandaa vizuri na tupo tayari kupangiwa yoyote kwenye robo fainali. Tunafahamu kwamba timu zote nne ni nzuri na ngumu ila na sisi tuna timu nzuri,”alisema Mwamnyeto.