Siri ya Simba Kambi Zanzibar Yafichuliwa...

Siri ya Simba Kambi Zanzibar Yafichuliwa...


Kikosi cha Wekundu wa Msimbazi Simba kimetua mjini Zanzibar tangu jana Jumanne (Machi 19) kikitokea jijini Dar es salaam, tayari kwa kambi ya juma moja kabla ya kuivaa Al Ahly ya Misri kwenye mechi ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku klabu hiyo ikieleza sababu ya kukimbilia visiwa hivyo vya karafuu.


Simba SC itakuwa mwenyeji wa mechi hiyo Ijumaa (Machi 29) Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ikihitaji kushinda ili kujiweka katika mazingira mazuri kabla ya mechi ya Mkondo wa Pili itakayopigwa jijini Cairo-Misri April 05.


Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema wameamua kuelekea kambi Zanzibar kwa ajili ya kupata utulivu ili kumpa muda Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha, kuandaa vizuri programu yake kwani alihitaji mazoezi yawe yanafanyika usiku kwani mechi zote mbili zitachezwa nyakati hizo.


Azam FC wanautaka ubingwa 2023/24 

“Watu wanajiuliza kwa nini Zanzibar? Tumeamua kwenda huko mahsusi ili kupata utulivu, kumpa muda mwalimu Banchikha kwa ajili ya kuandaa timu ya kwenda kumtoa Al Ahly na kwanza tumezingatia suala zima la utulivu, mwalimu anasema anahitaji programu ya mazoezi hasa nyakati za usiku kwa sababu mechi zote mbili ya Dar es salaam na Cairo zitachezwa usiku, tukakaa na kuona Zenji ndiko kuna miundomibu mizuri zaidi,” amesema Ahmed


Amesema wakiwa huko wanataraji kucheza mchezo mmoja wa kirafiki ili mwalimu aangalie kile ambacho amekitengeneza kama kimekuwa tayari, na baada ya hapo kikosi kitakuwa kimekamilika kuwavaa Al Ahly.


“Dhamira yetu safari hii ni kuitoa Al Ahly na kufuzu kwenda hatua ya Nusu Fainali, tuna vitu viwili, kumfunga na kumtoa, tushamfunga sana, kipindi cha miaka mitano tumekutana naye mara tatu, na imehusisha mechi sita, katika hizo tumeshinda mbili, ametufunga mbili na tumetoa sare mara mbili pia, kwa hiyo ukiangalia kitakwimu tunalingana, safari hii tunataka kutengeneza utofauti wa kumtoa na inawezekana, ndiyo maana tunataka kufanya maandalizi makubwa.” amesema meneja huyo


Tshabalala aweka matumani kwa Benchikha

Hata hivyo zipo taarifa kuwa kikosi kimepelekwa Zanzibar kufuatia ushauri wa wajumbe wa Baraza la Ushauri la Klabu, ambapo mmoja wa wajumbe wake, Ismail Aden Rage, alishawahi kushauri huko nyuma.


Baada ya kufungwa mabao 5-1 dhidi ya Young Africans na ilipokuwa inajiandaa kucheza dhidi ya Asec Mimosas, Rage alisema wakati wa uongozi wake alikuwa akiipeleka timu Zanzibar, hasa inapokuwa inakabiliwa na mechi ngumu.


“Natoa ushauri kwa viongozi wangu, wawakusanye wachezaji wawapeleke kambi Zanzibar, mimi wakati wa uongozi wangu niliwapa heshima sana watu wa Zanzibar, kila mechi kubwa nilikuwa nawapelekea timu, kule kuna nidhamu, huku tunasikia wachezaji mara wametoroka au hawataki kukaa kambini, huko huwezi kukuta mchezaji anatoroka kwenda Disco, hakuna ujinga wa namna hiyo.

Nunez ajiondoa Uruguay

“Kwa hiyo nashauri katika mashindano haya si lazima kwenda nje ya nchi kuweka kambi wala Dar es salaam, wawakusanye wachezaji wawapeleke kambini Zanzibar, wakirudi nakuhakikishia timu inakuwa fiti,” alishauri Rage Novemba mwaka jana, ambapo inasemekana ushauri huo pia umefikishwa kwa uongozi safari hii na umefanyiwa kazi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad