Februari 28, 2028 itakuwa siku ya Jumatatu. Wazungu walituletea jina la ‘Blue Monday’. Kama itaenda kila ilivyopangwa katika kifungo cha Paul Pogba, basi ndio siku ambayo atakuwa anamaliza kifungo chake cha kucheza soka.
Amefungiwa miaka minne na wahusika wa dawa za kuongeza nguvu michezoni. Kama ni kurudi atarudi akiwa na umri wa miaka 34. Kwa sasa ana umri wa miaka 30. Dunia imemuelemea Pogba. Sijui nini kimetokea katika maisha yake ya soka.
Kifungo hiki ni msumari wa mwisho katika maisha yake ya soka. Amekumbana na mengi lakini hili huenda likawa la mwisho kwake. Kama kila kitu kitakwenda sawa katika hili basi huenda huu ukawa mwisho wake katika soka.
Amedai kwamba atakata rufaa, lakini kama rufaa yake ikishindwa basi huenda huu ukawa mwisho wake katika kucheza soka. Unaweza kufikiria ni namna gani baada ya kufanya mazoezi peke yake kwa kipindi cha miaka minne halafu unarudi uwanjani ukiwa fiti?
Sidhani. Anaweza kurudi uwanjani kisha akajibanza katika timu yoyote ya katikati ya msimamo wa Ligi Kuu Ufaransa. Baada ya hapo hautazamii kwamba atarudi kuwa Pogba yule tuliyemfahamu. Hata kama asingefungiwa huu ndio ulikuwa wakati ambao Pogba alipaswa kuwa fiti huku akitazamiwa kuanza kurudi chini muda wowote kuanzia sasa.
Lakini ndio kwanza wakubwa wamesukuma nyundo katika maisha yake ya soka ambayo yamejaa vurugu nyingi. Vitu ambavyo Pogba atakumbukwa navyo ni kuvunja rekodi ya kuwa mwanasoka ghali zaidi duniani mwaka 2016.
Baada ya hapo, miezi 24 baadaye alitwaa Kombe la Dunia na Ufaransa pale Moscow, Russia. Kuanzia hapo maisha yake ya soka yamekuwa ni majanga tupu. Aliporudi klabuni kwake Old Trafford, kocha wake, Jose Mourinho alimuita Kirusi akiamini kwamba alikuwa ni mharibifu wa wenzake katika kambi ya Manchester United. Hawakuelewana tena.
Kabla mkataba wake haujamalizika Old Trafford wakala wake, Mino Raiola akafariki dunia. Huyu ni mmoja kati ya watu ambao walimpa pesa nzuri Pogba katika maisha yake ya soka. Ni yeye ndiye aliyemhamisha kutoka Manchester United kwenda Juventus akiwa mchezaji huru huku Sir Alex Ferguson akifura kwa hasira.
Ferguson alikuwa akiamini kwamba Pogba ambaye alikuwa kinda anayekuja juu angechukua nafasi ya Paul Scholes katika siku za usoni wakati huo Scholes akielekea ukingoni. Raiola alikuwa na mawazo mengine. Mpaka leo Ferguson anamchukia Pogba na si ajabu kwamba ameendelea kulichukia kaburi la Raiola.
Licha ya Raiola kufariki, miezi minne baadaye Pogba alifanikiwa kurejea tena Juventus Turin. Hata hivyo aliporejea tu Julai 2022 aliumia katika dakika ya 20 ya pambano lake la kwanza katika jezi za vibibi vizee hao wa Turin.
Kilichotokea ni kwamba majareha hayo yalisababisha akose kuipambania Ufaransa katika kutetea Kombe la Dunia pale Qatar. Fikiria kama Ufaransa ingeweza kutetea taji hilo katika pambano la fainali dhidi ya Argentina basi Pogba asingehesabika kuwa mmojawao.
Mwaka huohuo Pogba akaangukia katika janga la kifamilia. Kaka yake, Mathias Pogba pamoja na washkaji zake ambao walikuwa wanataka pesa kutoka kwa Pogba huku wakimtishia kutoa baadhi ya siri zake. Walikuwa wanataka kiasi cha Pauni 11 milioni. Aibu iliyoje!
Yaani ndugu zake mwenyewe wanataka pesa kutoka kwake ili wasimharibie siri zake. Siri gani? Kwamba Pogba alikuwa amekwenda kwa waganga wa kienyeji akitaka nyota ya Kylian Mbappe katika timu ya taifa ya Ufaransa ifunikwe na badala yake yeye ndiye awe staa zaidi.
Baadaye Pogba mwenyewe alikiri kwamba aliwahi kwenda kwa waganga kwa ajili ya kusaidiwa aepuke majeraha, lakini sio kwa ajili ya kufunika nyota ya Mbappe katika soka la Ufaransa. Kumbuka kwamba Mbappe ndiye mchezaji anayehusudiwa zaidi Ufaransa kwa sasa. Kesi hii ilimuacha Pogba akilalamika kwamba ni bora asingekuwa na pesa kwa sababu zimemtengenezea chuki na ndugu zake pamoja na rafiki zake. Pesa! Wakati wengine tunazitafuta kumbe kuna matajiri wanatazama wasingekuwa nazo. Alipopona majeraha yake Pogba alirudi uwanjani lakini alipogusa tu uwanjani katika pambano lake la kwanza tena akaumia ndani ya dakika 23. Alichanika msuli wake. Hadi wakati huu anafungiwa miaka minne Pogba alikuwa nje kwa majeraha. Na sasa amefungiwa miaka minne. Ni kama vile dunia imemuelemea. Vyovyote ilivyo nadhani hatukuwahi kumuona Pogba katika ‘peak’ yake ya hali ya juu. Katika umri wa miaka 30 hapa ndipo tulipaswa kumuona Pogba katika ubora wake.
Hata hivyo, maisha ya soka yamejazwa na mihangaiko mingi. Majeraha, kutopendwa na mashabiki, misiba, kusalitiwa na ndugu, kufungiwa na mengineyo. Hatujawahi kumfaidi Pogba ambaye ametulia uwanjani.
Kama Pogba angekuwa ametulia uwanjani na kuelekeza akili zake zote uwanjani basi anabaki kuwa mmoja kati ya viungo bora wa zama zake. Lakini kuna hatima ya baadhi ya wachezaji siku zote inakuwa kama hivi. Ni kama ilivyokuwa kwa Pogba. Ana mikasa mingi ndani na nje ya uwanja.
Nadhani kwa sasa tumeuona mwisho wake. Siamini kama itatokea Pogba akarudi kuwa yule tunayemfahamu kisha akarekebisha kila kitu. Muda hautampa nafasi. Anaweza kupunguziwa kifungo, lakini haitamsadia kitu katika umri ambao anao.
Kama angekuwa na miaka 23 huenda ingekuwa bado haujauona mwisho wa Pogba, lakini kwa sasa tumeuona mwanzo wa mwisho wake. alikuwa kiungo mwenye kipaji kikubwa lakini kulikuwa na maruweruwe mengi yaliyozunguka maisha yake ya soka.