Viungo Washika Mechi ya Azam na Yanga Leo, Vita ya Wafungaji Bora
Makali ya viungo katika kutengeneza nafasi na kufunga mabao yanategemewa kwa kiasi kikubwa kuamua mchezo wa Ligi Kuu baina ya Azam na Yanga itakayochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa leo kuanzia saa 2:30 usiku.
Wenyeji Azam wanamtegemea zaidi kiungo mshambuliaji wake Feisal Salum 'Fei Toto' ambaye anaingia katika mechi ya leo akiwa ndiye mchezaji wa Azam FC aliyehusika na idadi kubwa ya mabao akifanya hivyo mara 17 ambapo amefunga mabao 12 na kupiga pasi za mwisho tano.
Yanga yenyewe hapana shaka itamtegemea zaidi kiungo wake mshambuliaji Aziz Ki Stephane pia kwani ndiye mchezaji aliyehusika na idadi kubwa ya mabao akifanya hivyo mara 19 kwa kufunga mabao 13 na kupiga pasi sita za mabao.
Lakini ukiondoa Aziz Ki, Yanga ina Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya ambao kila mmoja amefunga mabao nane huku Pacome Zouzoua akiwa na mabao saba wakati kwa Azam FC, matumaini yao pia yapo kwa winga Kipre Junior anayeongoza kwa kupiga pasi za mwisho akiwa nazo nane.
Ushindi kwa Yanga leo, utaifanya izidi kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi ambapo itafikisha pointi 55 na hivyo kuhitajika kupata ushindi katika mechi nane zitakazofuata ili ijihakikishie ubingwa wa ligi pasipo kutegemea matokeo ya timu nyingine.
Lakini kama itapoteza, Yanga itajiweka katika hatari ya kuziruhusu Simba na Azam kupunguza pengo la pointi lililopo kati yao na hivyo kujiongezea ugumu kwenye mbio za ubingwa.
Kwa Azam FC, ushindi utaifanya ipunguze pengo la pointi kati yake na Yanga kubakia tano kwani itafikisha pointi 47 lakini itaishusha Simba kutoka nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
Azam imecheza mechi 13 mfululizo za Ligi Kuu bila kupoteza tangu ilipopoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya Namungo Oktoba 27 mwaka jana na hapana shaka itakuwa na hamu ya kufikisha mechi ya 14 leo wakati Yanga yenyewe inasaka mechi ya 16 ya ligi bila kupoteza kwani tangu ilipofungwa mabao 2-1 na Ihefu SC, Oktoba 4, imeshinda mechi 14 na kutoka sare moja kati ya 15 ilizocheza.
Misimu ya hivi karibuni mechi dhidi ya Yanga zimekuwa chungu kwa Azam FC ambapo mara kwa mara imejikuta ikipoteza iwe nyumbani au ugenini.
Kumbukumbu zinaonyesha katika mechi tano zilizopita za Ligi Kuu bara, Yanga imekuwa mbabe zaidi kwa Azam FC ambapo imeibuka na ushindi katika mechi nne na kutoka sare moja.
Katika mechi hizo tano zilizopita za Ligi Kuu, Yanga imefumania nyavu mara 12 huku Azam FC yenyewe ikifunga mabao saba.
Mara ya mwisho kwa Azam FC kupata ushindi mbele ya Yanga katika Ligi Kuu ilikuwa ni Aprili 25, 2021 pale ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Prince Dube ambaye katika mchezo wa leo atakosekana kwenye kikosi cha timu yake kwa vile amejiweka kando ya kikosi akilazimisha kuvunjiwa mkataba na klabu hiyo.
Kocha wa Azam FC, Youssouf Dabo alisema wao kama benchi la ufundi wamefanya kazi yao kwa usahihi kilichobaki ni wachezaji kufanya kazi yao huku wakitakiwa kutorudia makosa waliyoyafanya katika mchezo uliopita.
"Tunahitaji pointi tatu, sio rahisi lakini tumejiandaa kuhakikisha tunakuwa imara, lengo ni kuhakikisha tunapata ushindi ili kujirudisha kwenye ushindani wa kupagania taji," alisema.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema itakuwa mechi nzuri ya kuitazama kutokana na timu zote kuwa na mchezo mzuri na ameiona Azam ikiimarika tofauti na mzunguko wa kwanza.
"Tumetoka kucheza mechi ngumu mfululizo, naamini wachezaji wangu wana uchovu lakini hilo halitaondoa hali ya wao kupambana, wataingia kwa kuwaheshimu wapinzani," alisema Gamondi.