Kifo cha mwanafunzi wa darasa la kwanza, Jonathan Makanyaga (6), anayedaiwa kufariki dunia kwa kupigwa viboko na mwalimu, kimewaibua wadau wa elimu wakiiomba Serikali kudhibiti adhabu hizo ili kuepusha maafa kwa wanafunzi.
Wakizungumza na Mwananchi, wadau hao wamesema zipo njia mbadala za kutoa adhabu badala ya fimbo ambazo zinaweza kutumiwa na walimu.
Pia wameshauri walimu wenye tabia za kuadhibu wanafunzi na kuwajeruhi waondolewe kwenye taaluma ya elimu kwa kuwa kumfundisha mwanafunzi kwa viboko si kumjenga.
Mwanafunzi huyo, alifariki dunia Machi 10, 2024 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, (KCMC) alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi linawashikilia walimu tarajali watano kwa mahojiano kwa kudaiwa kuhusika na kifo hicho huku uchunguzi wa mwili uliokuwa umekamilika ukipangwa kurudiwa, kutokana na shaka iliyoibuliwa na familia ya mwanafunzi huyo.
Wadau wa elimu wa funguka
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wadau wa elimu wamesema utoaji adhabu wa walimu unapaswa kudhibitiwa ili kuepusha ukatili kwa wanafunzi.
Miongoni mwa waliozungumzia tatizo hilo ni Askofu Mstaafu wa Kanisa la Assemblies of God (TAG), Glorious Shoo aambaye amesema kumekuwepo na matukio ya ukatili unaoripotiwa wa wanafunzi kupewa adhabu zisizostahili.
"Kitendo cha kumchapa mwanafunzi ambaye alitarajia kufundishwa, kupendwa, kuelekezwa ni jambo ambalo linaonyesha mwisho au ukomo na uwezo wa mwalimu katika kumsaidia mtoto.
“Sisi tunaamini ya kwamba kitendo cha kumchapa mtoto kingelipaswa kuwa ni jambo la mwisho kuingia katika fikra ya mwalimu kwa sababu anazo nyenzo nyingi mno za kuweza kumsaidia mtoto," amesema Shoo ambaye pia ni rais wa Taasisi ya New life foundation mkoani Kilimanjaro.
Amesema mwalimu anazo njia mbadala nyingi za kumwelekeza mwanafunzi akae katika njia iliyosahihi, hivyo hapaswi kuwa na hasira ambazo zinaweza kuwadhuru wanafunzi.
"Ukimchapa mtoto ukiwa na hasira ni njia inayoonyesha kuwa unahamisha chuki badala ya upendo, kwa hiyo Serikali ifikirie hili, ziko nchi ambazo watoto hawachapwi shuleni na wana adabu nzuri tu na wanafaulu vizuri, hakuna fimbo kabisa na walimu wamekuwa marafiki wa watoto," amesema.
Amesema, mwalimu anayetumia fimbo ni aliyeshindwa na amekosa mbinu zote za kumweka mtoto sawa. Wengi wetu ni mashahidi, walimu waliokuwa wanachapa wanafunzi hawakuwahi kupendwa na watoto wengi wanafeli somo lao.
"Serikali inatakiwa kuchukua hatua hususani Wizara ya Elimu kwa sababu matukio haya yamekuwa yakijitokeza mara nyingi, wapo wanafunzi wanaokufa baada ya vipigo, hivyo ni wajibu wa Wizara ya Elimu kutoa maelekezo na kuchukua hatua kwa walimu ambao wanajichukulia sheria mkononi za kuchapa watoto."
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Fountain of Hope, Christina Mwiru amesema tukio la mwafunzi huyo limewaumiza na amewataka walimu kutumia njia mbadala za kutoa adhabu badala ya fimbo.
"Nimesikita sana na taarifa ambayo tumeipata, suala la kupiga watoto limekuwa ni kubwa na si zuri. Kiukweli unavyomchapa mtoto unatengeneza uadui mkubwa. Tutumie njia mbadala ya kumweleza hasara na mdhara ya hicho anachokifanya kwa kuwa bado anataka kujifunza, atajua kumbe nikifanya hivi ni kitu kibaya kuliko akikosea kidogo uanzane naye na fimbo bila kumweleza madhara ya hicho kitu," amesema Mwiru
Naye, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Christian of Hope, Mwalimu Gideon Gideon amesema matumizi ya viboko shuleni hayajengi urafiki baina ya mwalimu na mwanafunzi badala yake yanaandaa jamii ambayo itakuwa na kisasi.
"Walimu na wadau wa elimu tumepewa jukumu kubwa sana la kuandaa Taifa ambalo litaishi kwa upendo siku za mbeleni, kama tutatumia njia ambazo hazijengi urafiki na mwanafunzi, tunaandaa jamii ambayo itakuwa ya kisasi," amesema mwalimu huyo.
Atanas Joseph, mkazi wa Rombo, amesema suala la viboko shuleni limekuwa tatizo na kwaq hofu hiyo.
"Mimi ni shahidi kuna wanafunzi wengi wameacha shule kisa viboko, hebu walimu tafuteni njia mbadala ya kuadhibu hawa watoto, tunaenda kutengeneza Taifa la namna gani kama wanafunzi wanaacha shule kisa manyanyaso ya viboko, wazazi tunaumia pale tunapoona wanetu wanaacha masomo kisa mwalimu fulani," alisema.
Viboko mashuleni
Kwa mujibu wa Sera ya Elimu ya mwaka 2002 kifungu cha 3(1), adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima.
Kifungu kidogo cha pili kinasema adhabu ya viboko itatolewa kwa kuzingatia umri, jinsi na afya ya mwanafunzi na isizidi viboko vinne kwa tukio lolote.
Kanuni hiyo inampa namlaka mwalimu mkuu wa shule adhabu ya viboko au kukasimisha mamlaka yake “kwa umakini mkubwa” kwa mwalimu yoyote kutoa adhabu hiyo.