Wanachama 381 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Geita wametangaza kuachana na chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Uamuzi huo unakuja ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono aliyewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Geita kupitia Chadema, Upendo Peneza ambaye tayari ameshahamia CCM.
Wanachama hao wamepokelewa rasmi juzi kwenye mkutano ulioandaliwa na CCM mkoa kwa ajili ya kumpokea rasmi Peneza, uliofanyika katika viwanja vya Nyankumbu mjini Geita. Akizungumzia suala hilo, Peneza alisema yote hayo ni matokeo ya serikali iliyopo madarakani kusimamia ukweli na haki na yeye amechagua kuwa mkweli ndio maana amehamia CCM.
“Mimi sikutafutwa na mtu kuingia CCM, nimeomba mwenyewe kuwa mwanachama, kwa hiyo tangu taarifa nilipoitoa kwa viongozi wa CCM wamenipa heshima kubwa sana. “Rais Samia Suluhu Hassan anataka haki, mheshimiwa anataka kila mtu atendewe haki, ndiyo maana baada ya kuingia madarakani aliwatafuta ndugu zetu wa vyama vya upinzani.
“Anataka watu wahudumie watu kwa haki, wananchi wasionewe, kwa sababu huo ndio msingi wa uongozi wake, na kwa sababu hiyo na mimi nitajitahidi kutoa mchango wangu,” alisema.