Mkuu wa Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu, Faiza Salim amemuagiza Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamikoma, Kata ya Kabita Wilayani humo kuwaita Waganga wa tiba asilia Kijijini hapo ili kuwataka Wawachunge na kuwadhibiti fisi ili wasidhuru Watu kwakuwa fisi hao wanamilikiwa na baadhi ya Watu kijijini hapo.
DC ametoa agizo hilo wakati akiwa kwenye kikao cha kusikiliza kero za Wananchi Kijijini hapo ambapo Mwananchi Emmanuel Augustine amelalamikia uwepo wa fisi wanaosumbua Watu.
Akijibu hoja hizo DC Faiza amesema “Fisi wanamilikiwa na Watu, Mwenyekiti itisha Waganga wako wa tiba asilia wazungumze kuhusu fisi wawalinde fisi wao, lindeni fisi wenu wasilie Watu, mkiwaachia hivihivi mnamtisha Mzee Emmanuel anashindwa kufanya kazi nyingine kwasababu ya fisi”
“Mwenyekiti itisha Waganga wako wa tiba asili waambie wachunge fisi wao, Mimi sitaki kuingia mgogoro na wao kuanza kuwaua fisi wasije wakanifuata nyumbani kwangu, maana nikianza kuwaua hapa kuna DC alikuwa anawaua wanamfuata mpaka kwake Mimi sitaki malizana nao ukishindwa niite nije kuwaomba jaman lindeni zana zenu”